0


Na Gharib Mzinga.
Image result for mpira wa miguuKatika ulimwengu kuna Matukio mbali mbali ambayo yanabaki kama kumbukumbu kwa walimwengu, Matukio hayo hufanywa na binaadamu wenyewe ambao ndio wahusika wa ulimwengu huu, Tunaamini katika vitabu vya Dini ambavyo vinasisitiza kua binaadamu wote ni sawa, Lakini kuna baadhi yetu wamekua wakifanya mambo makubwa ya kuweza kubakia katika kumbukumbu za mamia ya watu wengine.
Katika ulimwengu huu Kuna mataifa mbali mbali na Yana historia zake, na huwenda zikawa mzuri au mbaya, Wapo Mashujaa wengi ambao wamefanya mambo makubwa kiasi kwamba Wamepeleka jamii zao kutoka sehem moja kwenda nyengine.
Tanzania katika Utawala bora haitokuja kumsahau Mwalimu Nyerere ambaye alipambana na wenzake katika kuleta Ukombozi Kwa Tanganyika. Huyu ni shujaa anayeungana na Mashujaa wengine wa aina yake kama vile Nelson Mandela, Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta, Kamuzu Bhanda na wengine.
Kuna Mashujaa wa muda wote ambao walikomboa jamii zao kifikra na kuzipeleka sehemu nyengine, Watu nao kama vile Martine Luther King Jr, Carl Marx, Aristotle, Plato, na Vilaadmir Lenin. Hawa wameukomboa ulimwengu kupitia mawazo yao ambayo yanatumika miaka mingi sasa.
Katika Vita kuna Mashujaa wengi sana ambao watakumbukwa na mataifa yao kama watetezi wa maslahi ya wengi, Ni vigumu kutomtaja mtu kama Hassan Bin Omar Makunganya. Huyu alipambana na serikali ya kijerumani miaka mingi iliyopita huko Wilayani Kilwa mkoa wa Lindi, Lakini Aliishia katika mikono ya Mabwenyenye hao na kunyongwa mbele ya Alaiki Mjini kilwa kivinje katika mwembe Kinyonga. Mtwa mkwawa alifanya Kama Makunganya, Utofauti yeye alifanyia Iringa kwa Wahehe wenzake.
Kinjekitile Ngwale Wa Ngarambe, huyu anabakia kua Shujaa namba moja kwa uwezo wake wa kuunganisha makabila zaidi ya 20 ili kupambana na serikali ya kijerumani Huko kusini mwa Tanganyika. Licha ya kutofanikiwa lakini wajerumani walipata somo kua hapa hawahitajiki.
Fashi Haijatuacha nyuma, Nayo imetuonesha Namna Mashujaa walivyokua bora katika kupambania Maendeleo ya jamii na ukombozi kwa ujumla, Kama hautoukumbuka ushujaa wa Odili wa Kitabu cha A man of the people kwa namna alivyoweza kupindua uongozi wa Chief Nanga, Basi utakumbuka Namna Mtolewa alivyokua na ushujaa wa kupindua utawala wa Bi kirembwe katika ardhi ya Giningi shahidi wa hili ni Saidi Mohammed wa Kivuli kinaishi.
Katika kandanda ulimwenguni, tunawapata Mashujaa wengi walioonekana hawapendwi katika nchi moja na kuthaminiwa kwao, Mashujaa hawa wamepeleka furaha kwa mataifa yao na bado kumbukumbu zao zipo na zitakumbukwa kizazi na kizazi. Wakati Luis Suarez akitukanwa na kulaaniwa katika majiji mengi ya Afrika kama vile Accra, Dakar, Abidjan, Bamako, Dar es salaam, kwa kuushika kwa makusudi mpira uliokua unapeleka Bara la Afrika katika nusu fainali ya kwanza pale Afrika kusini mwaka 2010. Lakini katika majiji mbali mbali ya Uruguay alisifiwa sana na kuitwa shujaa.
Zinedine zadane aliizamisha Brazil bora katika mchezo wa fainali ya kombe la dunia 1998 kwa kuifunga mabao mawili kwa sifuri, Hapa zidane aliitwa shujaa na itabakia hivyo kwa wakati wote, Hii ni sawa na lile Tukio la Diego Maradona kufunga bao la mkono alililipachika jina la  mkono wa Mungu, mwaka 1986 Katika dimba la Estadio Azteca Nchni Mexico na kupeleka Vilio katika majiji ya stoke, London, Bristol, Manchester, Cardiff na mengine mengi, huku Peter Shilton, Gary Lineker, na Peter Reid wakitoka vichwa chini. Tukio hili litabaki katika kumbukumbu kwa wakati wote.
Taifa la Tanzania katika Soka, limekua halina mafanikio kwa muda mrefu san. Mafanikio ya Nchi za Afrika na nyengine duniani katika kandanda ni kushiriki michuano mbali mbali na hata kama isipopata ubingwa. Kwa Afrika Mashindano makubwa ni Afcon ambayo huandaliwa na CAF. Mashindano haya Tanzania kwa miaka yote 56 ya Uhuru imeshiriki Mara moja tu Yale ya mwaka 1980 yaliyofanyika nchini Nigeria.
Mchezaji wa zamani wa Pan africa, Peter Augustino (Peter Tino) ndiye shujaa wa Tanzania aliyeipeleka nchi Hii kunako michuano hiyo, Ilikua mwaka 1979 katika mechi za kufuzu, Tanzania ilipangiwa na Zambia na mchezo wa kwanza ulipigwa Uwanjani wa Uhuru jijini Dar es salaam Tanzania iliibuka na ushindi wa goli moja kwa sifuri lililofungwa na Mohammed Rishard Adolph.
Mchezo wa pili Tanzania iliwafata Zambia Kwao katika Mji wa Ndola, huko Tanzania ilihitaji ushindi au sare ya aina Yoyote. Dakika za mapema Zambia wakapata goli la kuongoza ambalo lilidumu kwa dakika 86 ikiwa zimesalia dakika Tano mpira kumalizika Peter Tino alipokea mpira ulioanzia kwa Kipa Juma Pondamali baada ya kupangua mpira wa kona na Kuunganishwa na mlinzi kisiki Leodiger Tenga mpaka kwa kiungo Hussein Ngululu ambaye alipiga pasi ndefu kwa Peter Tino ambaye alitumia Nafasi vyema kwa kuweka wavuni mpira huo kwa pigo Kali kupitia guu lake la kulia uliomshinda mlinzi wa Zambia John Shileshi..
Kuanzia hapo hakuna mchezaji mwengine aliyeweza kufunga bao la thamani kama hilo ambalo liliipeleka Tanzania katika Afcon. Peter Tino anabakia kua shujaa wa Tanzania katika Soka, na mwaka huu 1980 unabakia kumbukumbu kwa historia ya kandanda ya taifa hili la Tanzania.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top