Mahakama
ya Wilaya ya Ilala leo Jumatatu Januari 22, 2018 imemhukumu Salum
Njwete maarufu kama ‘Scorpion’ kifungo cha miaka saba jela na kulipa
fidia ya Sh30 milioni itakayotakiwa kulipwa kwa haraka.
Akisoma
hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Flora Haule amesema ameridhishwa na ushahidi
uliotolewa na upande wa mashtaka, hivyo amemtia hatiani mshtakiwa chini
ya kanuni ya adhabu kifungu cha 225 kama kilivyofanyiwa marekebisho
mwaka 2007.
Haule
amesema kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imejiridhisha kumtia
hatiani Njwete kwa kosa la kujeruhi pamoja na wizi.
Baada
ya hakimu kumaliza kupitia hoja za pande zote mbili, wakili wa
Serikali Frank Tawali aliomba mahakama itoe adhabu stahiki kwa kuwa
Njwete alimtoboa macho, Saidi Mrisho ambaye alikuwa akitegemewa na
familia yake na Taifa.
Wakili
wa mshtakiwa, Hussein Hitu aliiomba mahakama kumpunguzia mteja wake
adhabu kwa kuwa ameshakaa rumande kwa muda mrefu, lakini pia ana familia
inayomtegemea.
Njwete (35) alikuwa akituhumiwa kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi ikiwemo kumtoboa macho Mrisho.
Post a Comment
karibu kwa maoni