NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji,
ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kutenga
fedha kwenye bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza ujenzi
wa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kondoa ili kukabiliana na changamoto
za afya zinazowakabili wananchi.
Dkt. Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa
Vijijini, ametoa maelekezo hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa
halmashauri ya Wilaya ya Kondoa wakati akianza ziara yake ya siku mbili
wilayani humo kukagua shughuli za maendeleo zinazotokana na fedha zilizotolewa
na Serikali ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya afya pamoja na miundombinu ya
elimu wilayani humo.
Alisisitiza kuwa atafuatilia na kuhakikisha kuwa mradi huo
unafanikiwa ili kusogeza huduma ya afya karibu zaidi na wananchi hususan
waishio vijijini ambao wanakosa huduma ya uhakika kutokana na kukosekana kwa
hospitali ya Halmashauri ya wilaya ya Kondoa.
Aidha, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji
amewataka watendaji wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha kuwa
wanawatumikia wananchi kwa moyo, umoja na mshikamano ili malengo ya kitaifa ya
kuwaletea maendeleo kupitia dhana ya Tanzania ya viwanda yaweze kufikiwa.
Alisema kila idara, ikiwemo ya kilimo, maji, elimu, afya,
maendeleo ya jamii na miundombinu ya barabara ihakikishe inatimiza malengo yake
ili wananchi waongeze uzalishaji hususan sekta ya kilimo itakayochangia
upatikanaji wa malighafi itakayotumika katika uzalishaji viwandani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Wialaya ya Kondoa Bw. Falesy Mohamed Kibassa ameahidi kuwa Halmashauri yake
imejipanga kuhakikisha kuwa malengo waliyojiwekea ya kuwatumikia wananchi wa
Wilaya ya Kondoa yanafikiwa kwa kuimarisha usimamizi na utendaji kazi katika
idara zote.
Alimhakikishia Dkt. Kijaji kwamba kwa kushirikiana kama timu
moja kati yake na watendaji wake, watahakikisha wanaifikisha wilaya hiyo kwenye
maendeleo yaliyokusudiwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni