Vilio,
simanzi na majonzi vimetawala kwa waombolezaji kutoka jijini Mwanza na
maeneo jirani wanaendelea na ibada ya mazishi ya mfanyabiashara Samson
Josia yanayofanyika nyumbani kwake mtaa wa majengo mapya wilaya ya Magu
mkoani Mwanza.
Mwili
wa mfanyabiashara huyo uliokutwa ukiwa umefungwa kwenye viroba ukielea
ndani ya Mto Ndabaka mpakani mwa wilaya za Bunda mkoa wa Mara na Busega
mkoani Simiyu umewasili asubuhi ya leo Machi 16 ukitokea Hospitali ya
Rufaa Mara ulikohifadhiwa kwa ajili ya uchunguzi tangu juzi.
Tangu
asubuhi, mamia ya waombolezaji kutoka jijini Mwanza na maeneo jirani
wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa marehemu wakitumia mabasi ya kampuni
aliyokuwa akimiliki.
Mabasi ya kampuni nyingine pia yanatumika kusafirisha waombolezaji kutoka jijini Mwanza bila malipo.
Marehemu
Josia aliyezaliwa mwaka 1968 alipotea tangu Februari 27 kabla ya gari
lake kukutwa likiwa limeteketezwa kwa moto ndani ya eneo la hifadhi ya
Taifa ya Serengeti mkoani Mara Machi 9.
Ibada
ya mazishi inaongozwa na Mchungaji Jackson Meza kutoka Kanisa la
African Inland Church of Tanzania (AICT) huku kwaya ya kanisa ambayo
marehemu alikuwa mfadhili wake ikiimba nyimbo za maombolezo.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara, Jaffari Mohamed, watu wanne
wanashikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano kuhusiana na kifo hicho
kilichoibua hofu na maswali yasiyo na majibu miongoni mwa ndugu, jamaa,
marafiki na wakazi wa jiji la Mwanza ambako marehemu alikuwa akiendesha
shughuli zake za kibiashara.
Post a Comment
karibu kwa maoni