0
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetolea ufafanuzi kuhusu kile kinachoitwa kutekwa kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Nchini TSNP, Abdul Nondo.

Akizungumza na Wandishi wa Habari Kamanda wa Kanda Maalumu, Lazaro Mambosasa amesema mnamo Machi 7, mwaka huu waliletewa taarifa kutoka kwa wenzao wa Iringa ambapo walithibitisha kupatikana kwa mwanafunzi huyo akiwa mzima huku akiwa hajaripoti kituo chochote cha Polisi.

Mambosasa amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalumu kwa kushirikiana na wenzao wa Iringa walithibitisha kuwa Nondo hakutekwa bali alijiteka ambapo mawasiliano ya jumbe za simu yake zinaonesha kuwa alikuwa akiwasiliana na mpenzi wake aliyepo mkoani humo.

 "Pengine alitaka kuzua hilo ili kujipatia umaarufu ila upelelezi uliendelea kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa hii ni baada ya kufanya uchunguzi wa kisayansi na kubaini muda ule aliosema ametekwa simu yake imeendelea kuonyesha mawasiliano aliyokuwa anafanya na huyo binti ambaye alikuwa amemfuata"

Mambosasa amesema kuwa walipomkamata walikuwa na mashaka kuwa huenda akawa amepatwa na ugonjwa wa malaria ya kichwa iliyopelekea kufanya hayo na kudai kuwa alipelekwa hospitali na kupimwa na kuonekana kuwa mzima asiye na matatizo yoyote ya kiakili.

"Alikuwa ni mzima wa afya njema na haya aliyafanya kwa makusudi kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, jeshi la polisi limebaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa huru baada ya kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alisafiri akiwa huru na akafika Iringa akiwa salama, kwa hiyo ni uzushi mtupu uliokuwa na malengo ya hovyo lakini kuna watu wengine walilishabikia jambo hili wengine huwezi kuamini kwa nafasi zao walilishabikia jambo hili la hovyo mtu kujizushia jambo" alisema Mambosasa na kuongeza;

" Jeshi la Polisi tunaendelea kutoa onyo kwa sababu hatutomuhurumia mtu yeyote ambaye anatafuta umaarufu kwa kuzua taharuki na wala hatutowapa nafasi ya kuharibu amani ya Nchi,"

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top