Serikali
imetaifisha dhahabu ya mabilioni ya shilingi na magari ya kifahari
kutokana na wahusika wake kukamatwa na kuhukumiwa kwa makosa ya rushwa
katika mwaka huu wa fedha.
Pia imetaifisha, pikipiki, mafuta, mashine za kuhesabia fedha na basi la abiria lililokuwa linatumika kusafirisha meno ya tembo.
Waziri
wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi, aliyasema hayo jana
alipowasilisha bungeni mjini hapa hotuba ya makadirio ya wizara yake kwa
mwaka ujao wa fedha.
Alibainisha
kuwa katika mwaka huu wa fedha, mali zilizotaifishwa kwa ujumla wake
zinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh. bilioni 5.685.
Waziri
huyo alisema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ilipokea majalada 683 ya tuhuma
za rushwa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru).
Prof. Kabudi alisema kati ya hayo, majalada 288 yaliandaliwa hati za mashtaka na 275 yalirudishwa Takukuru kwa uchunguzi zaidi.
Alisema majalada 115 yako katika hatua mbalimbali yakifanyiwa kazi na mengine matano yalifungwa.
"Washtakiwa
waliotiwa hatiani walipewa adhabu mbalimbali zikiwamo vifungo, faini na
mali kutaifishwa ambapo jumla ya Sh. bilioni 4.484 zilitozwa kama faini
kutoka kwa washtakiwa," alisema na kuongeza:
"Mali
zilizotaifishwa ni pamoja na kilogramu 24.5 za dhahabu zenye thamani ya
Sh. bilioni 2.012 na fedha za kigeni kutoka mataifa 15 zenye thamani ya
Sh.milioni 908.092.
"Mali
zingine zilizotaifishwa ni magari matano ya kifahari aina ya Range
Rover Vogue na moja aina ya Audi yaliyokamatwa katika Bandari ya Dar es
Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba, pikipiki 34, mafuta, mashine
za kuhesabia fedha na basi la abiria lililokuwa linasarifirisha meno ya
tembo."
Prof.
Kabudi alisema mwaka huu wa fedha pia mali za vyama vya ushirika vya
Mwanza (Nyanza Cooperative Union) na Shinyanga (Shirecu) zikiwamo
nyumba, viwanja na viwanda, zimerejeshwa serikalini kutoka mikononi mwa
watu ambao walizichukua bila kufuata utaribu wa kisheria.
Waziri
huyo pia alisema mwaka huu wa fedha kulikuwa na mashauri sita
yanayohusu ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi
yaliyoshughulikiwa.
Alisema
kuwa kati yake, mashauri manne yalikamilika kwa watuhumiwa kutiwa
hatiani na kuhukumiwa adhabu za kifungo cha kati ya miaka minne hadi 20
na mashauri mawili yaliyobaki yanaendelea kusikilizwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni