0


WAKAZI wa Kijiji cha Ntumba katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi 'wamemhukumu' mwenzao, Charles Sabuni (37) kucharazwa viboko 30 akiwa uchi hadharani au kulipa faini ya Sh milioni mbili taslimu baada ya kufumaniwa akizini na mke wa mtu nyumbani kwa mwenye mke.
Sabuni alipewa adhabu hiyo na wanakijiji wenzake baada ya kufumaniwa na mke wa mwakajijiji mwezao, Ntema Mwiwela usiku wa manane kijijini humo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda amethibitisha kutokea kwa mkasa huo huku akisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo.
Akisimulia mkasa huo Mwenyekiti wa kitongoji cha Ntumba, Samwel Mbuya amesema, tukio hilo lilitokea juzi, saa sita usiku nyumbani kwa Mwiwela.
Amesema, Mwiwela na mgoni wake ni majirani, wote ni baba wa familia wanaishi katika kijiji cha Ntumba wilayani Tanganyika na kwamba, baada ya majadiliano Sabuni alimrejeshea mwenye mke kiasi cha Sh 800,000 ikiwa ni gharama aliyotumia wakati akimposa mkewe.
Taarifa kutoka eneo hilo la tukio zinaeleza kuwa mchana wa siku hiyo ya tukio Ntemwa alimuaga mkewe kuwa ana safari ambapo ghafla alirejea nyumbani kwake saa sita usiku na kumkuta Sabuni akiwa chumbani kwake.
Baadhi ya majirani wa 'mgoni' huyo kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini walidai kuwa walipigwa na butwaa walipomshuhudia mwenzao Sabuni akiwa amewekwa chini ya ulinzi na Mwiwela chumbani kwake.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa kulipopambazuka, umati mkubwa ulikuwa umekusanyika katika eneo hilo la tukio.
Sabuni aliamuriwa atoke nje, wakamhukumu acharazwe viboko 30 hadharani akiwa uchi au alipe faini ya Sh milioni mbili taslimu.
Lakini aliokolewa na viongozi wa Seriikali ya kijiji na kitongoji waliofika eneo hilo la tukio na kuwazuia wananachi hao wenye hasira wasimuadhibu mwenzao kwa kumcharaza viboko 30 hadharani akiwa uchi kwa kuwa watakuwa wamekiuka haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji Ntumba, Mbuya kikao kiliitishwa kikiwashirikisha wazee na viongozi wa Serikali ya kitongoji pia alikuwepo Mwiwela na mgoni wake.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Sabuni aliamriwa alimlipe Mwiwela kiasi cha Sh milioni mbili,  aliomba apunguziwe adhabu hiyo, akaamriwa amrudishie mwenye mke (Mwiwela) Sh 800,000/- ikiwa ni gharama ya mahari aliyoitoa wakati alipomposa mkewe.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Sabuni alitoa kiasi hicho cha fedha ambazo alikabidhiwa Mwiwela ambaye baada ya kuzipokea fedha hizo alimkabidhi rasmi mke wake kwa Sabuni akisisitiza kuwa hawezi kuendelea kuishi naye.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top