Serikali
imeeleza kuwa inalinda thamani ya Shilingi kwa kudhibiti mfumuko wa bei ya
huduma na bidhaa, kuhamasisha usafirishaji na uuzaji wa bidhaa zilizoongezwa
thamani nje ya nchi kupitia program ya “Export
Credit Guarantee Scheme” na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za
Kigeni.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Viti
Maalumu Mhe. Devotha Mathew Minja aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa
kulinda thamani ya Shilingi kwa kuwa wapo wamiliki wa majengo ambao
wanapangisha majengo kwa kutumia fedha za kigeni kama vile Dola ya Kimarekani
badala ya fedha ya Kitanzania hivyo kusababisha kuendelea kuporomoka kwa
thamani ya shilingi.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa matumizi ya fedha za kigeni sambamba na
Shilingi ya Tanzania hapa nchini yanasimamiwa na Sheria ya Usimamizi wa Fedha
za Kigeni ya mwaka 1992 (The Foreign
Exchange Act, 1992), Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya Mwaka 2006 na Tamko
la Serikali la mwaka 2007 kuhusu matumizi ya fedha za kigeni kulipia bidhaa na
huduma katika soko la ndani.
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa mwezi Desemba 2017, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango (Mb), alitoa tamko kwa umma kuwa kuanzia Januari Mosi, 2018
bei zote hapa nchini zitangazwe kwa Shilingi ya Tanzania zikijumuisha kodi ya
nyumba za kuishi na ofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei ya
vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.
“Bei
ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza
kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za
kigeni, ambapo zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia
Tanzania, visa kwa wageni na gharama za viwanja vya ndege na hoteli, hata hivyo wageni hao wanapaswa
kutambuliwa kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili
kwa Kampuni”. Alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha aliongeza
kuwa viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka bei hizo
katika sarafu vinatakiwa kuwekwa wazi na visizidi vile vya soko, vilevile ni
benki na maduka ya fedha za kigeni pekee ndiyo yanayoruhusiwa kupanga viwango
vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.
Katika maswali ya nyongeza ya Mbunge huyo alitaka
kujua sababu zinazofanya baadhi ya Taasisi kuendelea kupata na kutoa huduma kwa
Dola, pia alihoji Serikali itapitia lini upya Sheria zake ili kuwa na sheria
itakayozuia matumizi ya fedha za Kigeni kama ilivyo kwa nchi ya Afrika Kusini.
Dkt.
Kijaji alisema kwa kuwa wajibu wa marekebisho na kupitisha Sheria ni wa Bunge hivyo basi, iwapo sheria iliyopo ina upungufu
ni vema kukafanyika maboresho kupitia Bunge.
“Ikumbukwe kuwa katika misingi ya Uchumi mambo
yanayosababisha kushuka au kudorora kwa thamani ya fedha yeyote duniani ni
pamoja na Nakisi ya Urari wa Biashara ambapo kwa Serikali ya Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa katika
kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini” alisema Dkt. Kijaji.
Post a Comment
karibu kwa maoni