Serikali
imeahidi kuboresha miundombinu na fursa nyingi za kiuchumi katika maeneo ya vijijini ili kuweka
mazingira bora na salama yatakayovutia wawekezaji katika sekta mbalimbali hususani Sekta ya Fedha.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kalenga
(CCM) Mhe. Godfrey Mgimwa aliyetaka kujua tamko la Serikali juu ya idadi kubwa
ya benki za biashara kufunguliwa kwenye miji mikubwa.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa miji
mikubwa inakidhi vigezo muhimu vya uwekezaji kwa Sekta ya Fedha kama vile uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi,
miundombinu ya kisasa na usalama ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.
Alisema
kuwa kufuatia mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi nchini unaotekelezwa tangu
mwanzoni mwa miaka ya 1990, shughuli nyingi za kiuchumi hususani benki
zinaendeshwa na Sekta Binafsi .
“Kwakuwa
Sekta Binafsi lengo lake ni kufanya biashara na kupata faida, uwanzishaji wa
huduma za kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia fursa za
kiuchumi zilizopo katika eneo husika, uwepo wa miundombinu wezeshi na usalama”,
alisema Dkt. Kijaji.
Alifafanua
kuwa Serikali inachokifanya ni kuweka mazingira bora yatakayowavutia wawekezaji
wa ndani na nje kuwekeza maeneo ya vijijini kwa kuwa lengo ni kufikisha huduma za kifedha kwa watanzania wote.
Katika
swali la nyongeza la Mbunge huyo, alitaka kujua mbinu mbadala ya Serikali
kuhakikisha inapeleka huduma za benki vijijini, kwa kuwa mpaka sasa Serikali bado
haijaunda Sera ya kuhakikisha huduma hizo zinawafikia walengwa hasa wa
vijijini.
Dkt.
Kijaji alieleza kuwa mpango mbadala wa kuhakikisha huduma za kibenki
zinafika vijijini upo na Serikali inausimamia vizuri, na kuongeza kuwa mpango
huo umeiwezesha Tanzania kuongoza katika huduma za fedha jumuishi barani
Afrika.
Post a Comment
karibu kwa maoni