Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine watano wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo, leo watafika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ukamilishaji wa masharti ya dhamana
waliyopata mwishoni mwa wiki iliyopita.
Machi
27, Mbowe na wenzake walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa nane, ombi lao la dhamana
likaahirishwa uamuzi kwa siku mbili ili Hakimu akajiridhishe.
Alhamisi,
Hakimu Wilbard Mashauri alikubali ombi la dhamana licha ya washitakiwa
kutokuwepo mahakamani siku hiyo kutokana na gari la kuwatoa mahabusu ya
Gereza la Segerea kuharibika.
Mbali
na Mbowe (56), washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter
Msigwa (52), Mbunge wa Kibamba John Mnyika (37), Mbunge wa Musoma Mjini,
Esther Matiko (41), Katibu Mkuu, Vincent Mashinji (45) na Naibu Katibu
Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu (39).
Hakimu
Mashauri alisoma masharti ya dhamana kuwa ni washtakiwa kujidhamini kwa
hati ya maneno ya Sh. milioni 20, wadhamini wawili kwa kila mshtakiwa
wanaotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini hati yenye thamani hiyo
ya fedha.
Aidha, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Mbowe na wenzake kukaa gerezani kwa siku saba.
Katika
kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya
Kawawa eneo la Mkwajuni Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja washtakiwa na
wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa
wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina
Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi
kujeruhiwa.
Shtaka
la tatu, ilidaiwa katika siku ya tukio la kwanza katika viwanja vya
Buibui vilivyopo Kinodnoni, Mbowe wakati akiwahutubia wakazi wa
Kinondoni, alitamka maneno ya uchochezi kuwa "Ninapozungumza hapa
kiongozi wetu wa kata ya Kinondoni Hananasif yupo mochwari... Amekamatwa
na makada wa CCM kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama...
Wamemnyonga, wamemwua halafu sisi tunaona ni jambo la kawaida...
Tunacheka na polisi... Tunacheka na CCM", alinukuliwa kwamba alitoa maneno hayo ya kuleta chuki na uchochezi kwa Watanzania.
Pia
shtaka la nne ambalo ni kosa la uchochezi na kusababisha chuki miongoni
mwa jamii, Jamhuri imedai Februari 16, mwaka huu katika mkutano wa umma
uliofanyika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni Dar es Salaam, Mbowe
alifanya uchochezi na kusababisha chuki kinyume na sheria kwa kutamka
yafuatayo:
"Tumejipa
kibali cha kutangulia mbele ya haki... haiwezekani wanaume wazima na
akili zetu na wake zetu na watoto wetu tukafanywa ndondocha.. hii ni
nchi ya ajabu. Mimi leo nipo hapa kulinda taifa... kule Afrika Kusini
Jacob Zuma amelazimishwa kujiuzulu... Robart Mugabe wa Zimbabwe
kang'olewa, kang'olewa Waziri Mkuu wa Ethiopia... juzi ameondoka kwa
people's power. Magufuli ni mwepesi kama karatasi".
Katika
shtaka la tano la uchochezi wa uasi linalomkabili Mbowe peke yake,
inadaiwa katika tarehe na maeneo hayo, alihutubia mkutano wa hadhara
akiwa na nia ya kupandikiza chuki na dharau kwa Watanzania dhidi ya
uongozi wa kisheria uliopo madarakani kwa kusema "Nitaongoza
mapambano nchi hii kwasababu tumechoka kuuawa... matokeo ya Watanzania
100 watakaokufa wataleta haki katika taifa hili. Wangapi wapo tayari
kuchukua bei hiyo?"
Katika
shtaka la sita la uchochezi wa uasi, wakili Nchimbi aliendelea kudai,
katika tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo mkoani Dar es Salaam, Mbowe
alitoa matamshi ya kupandikiza chuki na dharau kwa upande wa raia wa
Tanzania dhidi ya mamlaka halali kuwa; "Hii nchi inadharaulika...
imejengewa misingi wa uwoga, kwa lugha nyingine wanaume ni kama mademu,
si unawaona hao wanavaa suruali, waoga, bure kabisa... juzi ametekwa
kijana wetu, wanasema yupo mochuari, haki ya Mungu ingekuwa nchi
nyingine Kinondoni ingekuwa majivu... Lissu amepigwa risasi machine gun
na vyombo vya dola... Watanzania mnarudi nyuma... kuna mwandishi wa
habari leo ana siku 86 amebebwa na vyombo vya dola... suluhu ya nchi hii
haipo bungeni. Suluhu ya nchi hii ipo kwa wananchi wenyewe... lakini
ili tupate suluhu hiyo... ni lazima tukubali kubeba majeneza...
Inawezekana leo mnaogopa kufa... Ni bora tuwabebe wachache hata wakiwa
200 waliokufa katika ukombozi ili hatimaye nchi hii isimame kama nchi ya
wanaume wengine katika dunia hii".
Katika
shtaka la saba la kushawishi kutendeka kwa kosa la jinai , inadaiwa
katika tarehe hiyo hiyo na maeneo hayo, Mbowe alishawishi wakazi wa
Kinondoni kutenda kosa la kufanya maandamano na mkusanyiko usio halali.
Katika
shtaka la nane la kushawishi utendaji wa kosa la jinai, linalomkabili
mshtakiwa wa pili Msigwa, ilidaiwa katika maeneo hayo hayo Msigwa
alishawishi raia na wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa
kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.
Post a Comment
karibu kwa maoni