Tanzania imeendelea
kuaminiwa na Jumuiya ya Kimataifa ambapo Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Falme
za Kiarabu-Abu Dhabi, umeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za
Marekani milioni 15, sawa na shilingi bilioni 34 za Tanzania, kwa ajili ya
kuboresha barabara ya Uvinza hadi Malagarasi yenye urefu wa kilometa 51, kwa
kiwango cha lami
Hafla fupi ya uwekaji
saini wa mkataba huo imefanyika katika makao makuu ya Mfuko huo yaliyopo Abu
Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambapo Mhandisi Mussa Ibrahim Iyombe,
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI,
amesaini kwa niaba ya Serikali, na Mhe.
Mohamed Saif Al Suwaidi Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa niaba ya Mfuko huo.
Akizungumza baada ya
kusaini Mkataba huo, Katibu Mkuu-TAMISEMI, Mhandisi Mussa Iyombe, amesema kuwa
barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa ni kiungo kikuu cha usafiri wa abiria na mizigo
kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kigoma na nchi jirani za Burundi na
Kongo DRC.
Amesema kuwa uamuzi
wa Serikali wa kuboresha barabara hiyo kwa kiwango cha lami umelenga kuchochea
uchumi wa nchi kwa kuwezesha usafirishaji wa mazao ya wakulima pamoja na kupunguza
gharama na kuongeza uwezo wa kufanya biashara na nchi hizo jirani.
"Tutabakiwa na
kipande cha barabara yenye urefu wa kilometa 28 kutoka Urambo hadi Kaliua na
kilometa 42 kutoka Chagu hadi Kazilambwa, barabara ambazo Serikali inaendelea kuzitafutia
fedha ili kukamilisha barabara yote inayoelekea ukanda huo wa kati kutokea Dar es Salaam, Manyoni (Singida), Tabora hadi Kigoma"
Alisema Mhandisi Iyombe.
Ameushukuru Mfuko huo
kwa kuendelea kuiamini Serikali na kutoa mkopo huo wenye masharti nafuu baada
ya kufanya hivyo hivi karibuni kwa kutoa mkopo mwingine wa dola milioni 57, uliofanikisha
kuboreshwa kwa barabara ya Kidahwe hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 77 kwa
kiwango cha lami.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Mhe. Mohamed Saif Al Suwaidi, kwa upande wake,
amesema kuwa Mfuko huo uko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Amefafanua
kuwa mradi huo ambao mkataba umesainiwa mjini Abu Dhabi, utakuwa ni wa nne
kufadhiliwa na Mfuko wake Tangu uhusiano wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)
na Tanzania uanzishwe mwaka 1977, ukiwemo mradi wa kuendeleza kiwanda cha Sukari cha
Kagera, Mradi wa Maji Vijijini huko Viwani Zanzibar na Mradi wa kuboresha barabara ya
Kidahwe hadi Uvinza kwa kiwango cha lami.
Kwa upande wake, Balozi
wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk amesema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni
kiashiria cha kukubalika kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli, katika kuwaletea wananchi wake maendeleo ya haraka na
kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.
"Hatua hii ni
uthibitisho wa mahuasiano mazuri ya kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na
Umoja wa Falme za Kiarabu uliodumu kwa muda mrefu tangu mwaka 1977" Alisisitiza Mhe.Mbarouk
Mhe. Mbarouk
amebainisha kuwa kukamilika kwa barabara hiyo ya Uvinza hadi Malagarasi
kutachochea maendeleo ya kiuchumi na mapinduzi ya viwanda kwa kuunganisha
shughuli za kiuchumi kama vile kilimo na maliasili pamoja na kukuza utalii.
Post a Comment
karibu kwa maoni