0
Naibu Waziri wa Nchi, Ofi si ya Makamu wa Rais, Muungano na Mzingira, Kangi LugolaNAIBU Waziri wa Nchi, Ofi si ya Makamu wa Rais, Muungano na Mzingira, Kangi Lugola amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini, kuorodhesha vyanzo vyote vya maji, vinavyopatikana katika maeneo husika ili vitambulike na kutunzwa.
“Tunapiga kelele wakurugenzi leteni orodha za vyanzo vya maji katika maeneo yenu, lakini ni wachache wanaoleta. Natoa wiki mbili kazi hii iwe imekamilika na wale watakaoshindwa kutekeleza agizo hili nitajua pa kuwapeleka,” alisema Lugola. Akizungumza katika ziara ya kukagua uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji mto Ngerengere mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki, Lugola alisema wakati umefika kwa watendaji wa serikali wasiotekeleza maagizo, kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.
Lugola aliyetembelea pia Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Kampasi ya Mazimbu, ambayo eneo kubwa liliharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni, alisema agizo hilo lilishawahi kutolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, lakini halijatekelezwa na ndiyo maana matatizo kama hayo yanajitokeza.
“ Nimekuwa na mashaka na ndio maana narejea aliyoyatamka Mheshimiwa Rais wakati anaongoza Mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kwamba inaonekana watendaji wengi aliowateua hawajamuelewa. Kwa hiyo hadi wiki mbili zikiisha hamjatekeleza agizo hili, nitayapeleka majina yenu kwake ili aamue kama vitumbua vyenu avitie mchanga ama la,”alisema Lugola.
Naibu Waziri huyo alisema uharibifu wa vyanzo vya maji aliouona, wasipochukua hatua za haraka SUA ambayo mbali ya kutoa wanataaluma inalinda pia historia ya wapiganaji wa chama cha ANC cha Afrika Kusini, itapotea. “Tumejionea namna mafuriko makubwa yalivyoathiri miundiombinu ya mabweni na nyumba za walimu na kuhatarisha maisha ya wanafunzi, SUA sehemu ya Mazimbu; na si tu kwa maana ya miundombinu, bali ni pamoja na historia ya wenzetu wa Afrika Kusini,” alisema Lugola.
Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda alisema miaka ya nyuma walikuwa wakipata mafuriko, lakini kutokana na shughuli za uchimbaji mchanga mafuriko ya mwaka huu, yamekuwa makubwa na kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wakufunzi pamoja na majengo. “Tuna eneo la shamba la chuo, hatukuwa tukiweza kufika kule kuna wanafunzi wetu wanne walitoka shambani wakazolewa na maji lakini kwa bahati madaktari walikuwa karibu, tukaokoa maisha yao.
Tulijitahidi kutafuta katapila kupanua mto ili walau kupunguza athari,” alisema Profesa Chibunda. Aliongeza kuwa: “Tunaamini ujio wako unaweza kuleta mwanga ili kuwa na juhudi za pamoja ili eneo hili lisalimike kwa sababu tusipofanya chochote ndani ya miaka miwili tutafunga chuo, hapa kuna wanafunzi 9,300 na zaidi ya 400 wanakaa kwenye Kampasi ya Mazimbu.”

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top