Mbunge
wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza amemtaka Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Mwigulu Nchemba kulieleza Bunge sababu za wabunge wa Viti
Maalum kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo wanayotokea.
Peneza
amesema kama kweli Dk Mwigulu anataka kuwa Rais wa Tanzania siku
zijazo, akishindwa kulishughulikia jambo hilo atakuwa amepoteza sifa
hiyo kutokana na kuzima ndoto za wanawake na vijana.
Akichangia
bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2018/19 Peneza alisema polisi
wamekuwa wakikandamiza demokrasia, ikiwamo kuwazuia kufanya mikutano
kwenye mikoa yao.
“Kaka
yangu, Mwigulu kama ulitegemea kuwa Rais siku moja, wabunge wa viti
maalum wapo humu kwa mujibu wa Katiba ambayo inazungumzia uwepo wa
wabunge wa viti maalum ambao majina yao yanapendekezwa na vyama vyao,”
alisema Peneza.
“Lakini
mimi pamoja na wabunge wengine tumekuwa tukizuiwa kufanya mikutano ya
hadhara, wabunge tunaambiwa tufanye kazi nyumbani? Wabunge wa viti
maalum tunadhalilishwa, mtuache tufanye kazi.”
Alisema,
“Kwa nini tunalipwa fedha, tunahitaji tufanye mikutano kwani tunalipwa,
lazima tuwasikilize wananchi na turuhusiwe kufanya mikutano katika
maeneo yetu na mwisho tutasema Serikali ya awamu ya tano haitaki
wanawake wafanye siasa.”
Alisema kupitia mikutano ya hadhara ndiko ambako wanaibuka wanawake na vijana akiwamo yeye.
Post a Comment
karibu kwa maoni