Serikali
imewasisitiza wananchi kuacha matumizi ya mkaa na badala yake watumie
nishati nyingine ili kuepuka changamoto za uharibifu mkubwa wa mazingira
unaoendelea kote nchini kutokana na matumizi ya mkaa.
Msisitizo
huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya
Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika Juni 5 mwaka huu.
Waziri
Makamba alisema kuwa maadhimisho hayo kitaifa yatafanyika Jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kuwapa fursa wananchi wa Jiji la Da re Salaam
kuelimishwa na kuhamasishwa kupambana na changamoto za uharibifu wa
mazingira unaolikumba jiji hilo ikiwemo mafuriko, uchafuzi wa mazingira
utokanao na plastiki, kubomoka kwa kuta za fukwe za Bahari ya Hindi
pamoja na utumiaji wa kiasi kikubwa cha nishati ya mkaa.
“Nasisitiza
kwamba, sote tuna jukumu la kuanza kubadilika kutoka kwenye matumizi ya
mkaa na kuanza kutumia nishati mbadala wa mkaa. Tukumbuke kwamba suala
la kuhifadhi mazingira ni jukumu letu sote na tunapaswa kulitekeleza kwa
vitendo,” alisema Makamba.
Waziri
Makamba alieleza kuwa matumizi makubwa ya mkaa hayapo tu katika Jiji la
Dar es Salaam bali pia yapo katika maeneo mengine ya nchi, hivyo
kutokana na matumizi makubwa ya nishati hiyo, maadhimisho ya kitaifa
yataongozwa na Kaulimbiu inayosema; “Mkaa Gharama; Tumia Nishati
Mbadala”.
Alibainisha
kuwa takwimu zinaonyesha kwamba mpaka mwaka 2017 kiasi cha hekta 46,942
za misitu huharibiwa kila mwaka kwa ajili ya kupata mkaa ambapo
matumizi makubwa yako katika miji mikubwa ikiwemo Dar es Salaam, ambako
wastani wa tani 500,000 za mkaa hutumiwa kila mwaka.
Waziri
Makamba alieleza kuwa uharibifu wa misitu unasababisha kuwepo kwa
changamoto nyingine za mazingira kama vile ukame, majangwa, uharibifu wa
ardhi, upotevu wa mimea asilia, upotevu wa viumbe hai mbalimbali,
upungufu wa upatikanaji wa maji na upungufu wa uzalishaji kwenye kilimo.
“Kutokana
na changamoto hizo, wakati wa wiki ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira
Duniani, kutakuwepo maonesho ya nishati mbadala wa mkaa na teknolojia
zake. Maonesho haya yatafanyika katika viwanja vya mnazi mmoja kuanzia
Mei 31 hadi tarehe Juni 5, 2018,” alisema Makamba.
Alieleza
kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na Kongamano la Mazingira,
Mabadiliko ya Tabianchi na Uchumi litakalofanyika Juni 1, 2018,
Kongamano la viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali litakalofanyika
Juni 2, 2018 pamoja na kongamano la wananchi wa Mkoa wa Da res Salaam
litakalofanyika tarehe 3 Juni, 2018 katika viwanja vya Zakhem Mbagala.
Aidha
Waziri Makamba alitoa wito kwa mikoa mingine yote nchini kushiriki
kikamilifu katika maadhimisho hayo kwa kuhamasishana, kelimishana
masuala yahusuyo hifadhi ya mazingira.
Tarehe
5 Juni, 2018 watanzania wataungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha
Siku ya Mazingira Duniani. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira yaliamuliwa
mwaka 1972, katika mji wa Stockholm nchini Sweden, kwenye mkutano wa
kwanza wa Umoja wa Mataifa uliohusu Mazingira.
Mwaka
huu maadhimisho hayo kimataifa yatafanyika nchini India katika mji wa
New Delhi. Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho hayo ni “Beat Plastic
Pollution” ambayo inahimiza jamii kuepuka uchafuzi wa mazingira utokanao
na plastiki.
Post a Comment
karibu kwa maoni