0
MENEJIMENTI ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imetoa ufafanuzi wa ongezeko la bei za matibabu na kusema kwamba halitaathiri michango ya wanachama wake na kwamba imelenga kuboresha zaidi huduma wanazopatiwa wanachama wanapotafuta msaada wa tiba katika vituo vilivyosajiliwa na mfuko huo.
Aidha, menejimenti hiyo imesema kwamba bei mpya ambazo zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 13 zimeridhiwa baada ya majadiliano ya muda mrefu.
Imesema mabadiliko yaliyotokea ya kuboreshwa kwa bei yamelenga kutanua wigo huduma na uwezeshaji, ikiwamo za upasuaji na ada ya kumwona daktari huku pia wakiongeza fao la vipimo na matibabu ikiwemo upasuaji wa magonjwa ya moyo nchini.
Akizungumza Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bernard Konga alisema majadiliano ya kufanya mabadiliko ya bei hizo yaliyofanyika kwa miaka miwili na kushirikisha wadau mbalimbali, yapo maeneo ambayo gharama zimeongezeka, mengine kupungua lakini pia kukiwa na maeneo ambayo hayajaguswa kabisa kutokana na mifumo na sera za afya za nchi.
Mkurugenzi huyo akifafanua zaidi alisema si kweli kuwa mabadiliko hayo yametokana na Mfuko huo kushindwa kulipa watoa huduma kama inavyodaiwa bali ni kutokana na tafiti zilizoonesha kuwepo kwa haja ya kufanyika mabadiliko kukidhi mahitaji ya matibabu bora kwa wanachama wake na kuondoa utofauti katika malipo.
Alisema kama mfuko huo ungekuwa na tatizo usingeweza kulipa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka wa fedha 2015/16 kwa kuhudumia wahitaji 6,505,492. Aidha alisema kwamba wana uwezo wa kuhudumia wanachama wake kwa miaka minne ijayo bila michango zaidi.
Akizungumzia mabadiliko yaliyofanywa kwenye maboresho, alisema nia ilikuwa kubadilisha mfumo wa ulipaji, ikiwemo ada ya kumuona daktari ili kuondoa mfumo wa awali uliokuwa na viwango tofauti vya ada kwa mgonjwa anayehudhuria hospitali kwa mara ya kwanza na anaporudi kwa mara nyingine.
“Kwa sasa ada hii inalipwa kwa viwango sawa ambapo Mfuko unalipia kadri ya uhitaji na pia upasuaji umeainishwa kutokana na aina yake kama mdogo, mkubwa au wa kitaalamu,” alisema.
Konga alisema Mfuko huo unatekeleza sera, miongozo na taratibu zilizowekwa na serkali na kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, hivyo vituo vilivyosajiliwa na Mfuko vina ngazi tofauti na hivyo bei za huduma zinaruhusiwa kulipwa kutegemea na daraja la kituo husika.
Hadi kufikia Juni, mwaka huu, vituo vilivyosajiliwa na Mfuko vilikuwa ni 6,439, kati yake vya serikali vikiwa 5,091, madhehebu ya dini 572 na binafsi 776. Alisema dawa na vipimo ndivyo vinalipwa sawa katika ngazi zote za vituo, huku mabadiliko ya tofauti yakiwa katika ukubwa wa taaluma.
Alisema kutokana na kuwa Mfuko umeingia Mkataba na watoa huduma kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanachama wake, endapo mwanachama atakataliwa kupewa huduma hatua za kisheria zitachukuliwa na ikiwa madai yanatokana na udanganyifu hayatalipwa.
Aliwataka wanachama wanapopata matatizo kuhusu madai yoyote yale katika tiba zao kupiga simu ya bure 0800 110063.
Alisema katika kipindi cha mpito cha maboresho hayo kinachoanzia Julai hadi Desemba, mwaka huu wataendelea kupokea maoni na malalamiko hususani suala la vipimo ambalo linalalamikiwa sana na baadhi ya watoa huduma baada ya Mfuko huo kuamua kulipa gharama moja kwa watoa huduma wote.
Maeneo yaliyoboreshwa zaidi Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kitaalamu za Matibabu wa NHIF, Dk Aifena Mramba akizungumzia faida za maboresho alisema baada ya vipimo na upasuaji wa moyo kuanza kufanyika nchini wameongeza fao la matibabu ya magonjwa hao.
Dk Mramba alisema kwa huduma za upasuaji wameongeza kwa asilimia 100 na kutoa mfano kwa upasuaji wa uzazi iliokuwa unalipiwa Sh 130, 000 sasa ni Sh 350,000. Alisema pia upasuaji wa kufunga mirija ya uzazi na kidole tumbo uliokuwa umetengewa Sh 130,000 tu sasa umeongezewa fedha hadi Sh 300,000.
Maboresho mengine ni ada ya kumuona daktari ambapo Mramba alisema tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kwa Hospitali za Mikoa walikuwa wakilipwa Sh 2,000 sasa watalipwa Sh 15,000 huku Hospitali za Wilaya ambako walikuwa wakilipa Sh 1,000 kama ada ya kumuona daktari sasa watalipwa Sh 10,000.
Alisema Mfuko wa NHIF unasimamia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wanufaika wake ambao ni zaidi ya milioni 3.3 wanaopata matibabu katika vituo 6,400 nchi nzima.
Ufafanuzi huo wa NHIF umekuja baada ya kuwepo kwa taarifa zinazoleta mkanganyiko kwa wanachama wa Mfuko huo kwamba umepunguza malipo kwa asilimia 60, hatua iliyoonekana kutishia wanufaika kukosa huduma

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top