Benny Mwaipaja, WFM
Serikali imesema inaendelea kupitia sheria, kanuni
na taratibu za misamaha ya kodi mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha kuwa misamaha
yote isiyokuwa na tija inafutwa na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza mapato
kwa ajili ya kupeleka huduma za maendeleo kwa wananchi wake.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu
swali la Msingi la Mbunge wa Masasi, Mhe. Rashid Mohamed Chuachua (CCM),
aliyetaka kujua namna Serikali inavyodhibiti misamaha ya kodi tangu irekodiwe
kwa viwango vya juu Mwaka wa Fedha 2011/2012.
Mhe. Chuwachuwa alihoji mwenendo wa utoaji wa
misamaha ya kodi kwa wawekezaji kwa maelezo kuwa Tanzania imekuwa miongoni mwa
nchi zilizopoteza fedha nyingi kwa ajili ya misamaha ya kodi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kigezo
cha kuvutia Wawekezaji.
Alisema kuwa kwa mujibu taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2009-2010, Tanzania ilipoteza
asilimia 15 ya Pato la Taifa lililotarajiwa kukusanywa kutokana na misamaha ya kodi,
mwaka 2010-2011 asilimia 8, kwa mwaka 2011-2012 asilimia 27 ya mapato ya Serikali
yalipotea.
“Je hali ya misamaha ya kodi kuanzia 2013-2014 hadi
sasa ikoje’’. Alihoji Mhe. Chuachua.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), misamaha ya kodi kama sehemu ya asilimia
ya Pato la Taifa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013/14 hadi sasa imekuwa
ikipungua mwaka hadi mwaka.
“Misamaha hiyo ilikuwa asilimia 2.2 ya Pato la
Taifa mwaka 2013/14, asilimia 1.9 ya Pato la Taifa katika mwaka 2014/15 na
asilimia 1.1 ya Pato la Taifa katika mwaka 2015/16” Alifafanua Dkt. Kijaji.
Aidha aliongeza kuwa misamaha ya kodi
ikilinganishwa na mapato ya kodi imekuwa ikipungua kutoka asilimia 18 ya mwaka
2013-2014 hadi kufikia asilimia 8.6 ya mapato yote ya kodi katika mwaka
2015-2016.
Dkt. Kijaji alifafanua kuwa misamaha ya kodi
inatolewa na Serikali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi zilizopo,
huku kukiwa na baadhi ya huduma zinazotolewa katika jamii ambazo hazistahili
kulipiwa kodi kwa sababu hazina manufaa ya kibiashara.
‘’Pamoja na hatua nzuri zinazochukuliwa na Serikali
za kupunguza misamaha ya kodi ni vema ikafahamika kwamba si kila msamaha wa
kodi una madhara hasi katika jamii na uchumi kwa ujumla’’. Alisema Dkt. Kijaji.
Alitolea mfano wa mashirika ya dini yanayopata
misamaha ya kodi kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)
(2014), kwa sababu huduma zinazotolewa na taasisi hizo hazina faida ya
kibiashara kama ilivyo kwa kampuni za kibiashara.
Katika swali la nyongeza Mbunge huyo, alitaka kujua
mpango wa Serikali kuhusu misamaha ya kodi kwa mwaka wa fedha 2017-2018.
Post a Comment
karibu kwa maoni