Benki ya NMB imepata faida ya ya
shilingi bilioni 153.8 kwa mwaka 2016 hivyo kuiwezesha kutoa gawiwo la shilingi
bilioni 16.5 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 32 ya hisa za Benki hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Mpango (Mb) alikabidhiwa hundi
kifani ya gawiwo hilo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa wanahisa wa Benki hiyo
uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mpango amezipongeza juhudi za watendaji wa Benki hiyo
waliofanikisha kupatikana kwa faida iliyowezesha Serikali kupata gawiwo. Aidha,
Serikali inajivunia mafanikio makubwa ya kiutendaji ya NMB na uwekezaji wake ambao
unatija na unaifanya serikali isijutie uamuzi wake wa kuibinafsisha Benki hiyo.
Amesema fedha hizo zilizopatikana kutokana na gawiwo zitaelekezwa
kwenye maendeleo ili kutatua baadhi ya kero zinazowakabili wananchi.
Ameahidi kuwa, Serikali kama mwanahisa itaendelea kuitumia Benki hiyo
kikamilifu katika huduma za kibenki ili kuiwezesha kuongeza mapato.
“Shughuli ambazo Serikali itazifanya kupitia NMB Bank Plc ni pamoja
na malipo ya mishahara ya wafanyakazi wa
Umma na pia kukusanya mapato ya Serikali yanayotokana na kodi na yasiyo ya
kodi.
Waziri Mpango ametumia nafasi hiyo kuagiza kampuni ambazo zenye ubia na
Serikali kuiga mfano wa NMB Benki Plc na kupeleka gawiwo katika faida wanayopata.
“Katika Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli haiingii akilini kusikia kila mwaka mnapata hasara lakini mpo hamtoki,
tumevumilia vya kutosha sasa imetosha, haiwezekani unawekeza miaka 10 lakini
watanzania hawapati chochote” alionya Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Ineke Bussemaker
amesema jumla la gawiwo lote litakalolipwa kwa wanahisa ni shilingi Bilioni 52
kiwango ambacho kinaendana na sera ya Benki ya kutoa theluthi moja ya asilimia
33.3 ya faida baada ya kodi kwa wanahisa wake.
Bussemaker alisema kuwa mafanikio ya Benki hiyo katika mwaka ulioishia Disemba
31,2016 ilipata faida ya shilingi bilioni 153.8
licha ya changamoto za kibenki, likiwa ni ongezeko la asilimia 2,
ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo ilipata faida ya shilingi bilioni 150.3
Wanahisa wa Benki hiyo wamekubaliana kubadili jina la Benki hiyo kutoka
National Microfinance Bank na kuwa NMB Bank Plc. Waziri mpango amesema
mapendekezo ya kubadili jina yalifika Serikalini na Serikali imeridhia.
Post a Comment
karibu kwa maoni