Ndugu
wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwiline aliyepigwa risasi na Polisi Februari 16, 2018 wameeleza ndugu
yao alifariki dunia baada ya kupigwa risasi kichwani.
Wametoa
ufafanuzi huo leo Februari 19, 2018 muda mfupi baada ya kususa kupokea
mwili wa mwanafunzi huyo uliokuwa ukifanyiwa uchunguzi Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH) bila kuelezwa nini kilichomuua.
Wakizungumza
mara baada ya maafikiano baina yao na madaktari, wamesema wamepewa
sehemu ya ripoti ya uchunguzi ambayo wameridhika nayo na sasa wanakwenda
kufanya kikao cha ndugu kujadili namna gani watampumzisha Akwilina.
Shemeji
wa mwanafunzi huyo, Festo Kavishe amesema uchunguzi wa mwili huo,
umeonyesha kwamba Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.
"Ripoti
ambayo tumepewa imeonyesha kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa
vibaya na risasi ambayo iliingilia upande wa kushoto kwa kichwa chake na
kutokea upande wa kulia ambao umefumuka vibaya," amesema.
Kwa
mujibu wa Kavishe, iwapo madaktari wasingewapatia majibu hayo
wasingethubutu kuuchukua mwili huo kwa mazishi, kwa sababu walihitaji
kupata picha kamili ya nini kilimuua Akwilina.
"Sasa
tumeshafahamu nini hasa kimemuua ndugu yetu kwa mujibu wa ripoti
iliyotolewa na madaktari baada ya uchunguzi, hivi sasa tunakwenda
kujadiliana kuhusu mazishi yake," amesema Kavishe.
Akwilina
alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani
akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni
wafuasi wa Chadema.
Post a Comment
karibu kwa maoni