0
RIPOTI ya uchunguzi maalumu uliofanywa na Umoja wa Mataifa (UN) kufuatia shambulizi lililosababisha vifo vya askari wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mwishoni mwa mwaka jana imebainisha lilifanywa na waasi wa Alliance of Democratic Forces (ADF).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na UN, ushahidi uliopatikana unaonesha ADF ndio walifanya shambulizi hilo la kushtukiza na kusababisha vifo vya askari hao. Januari 5, mwaka huu, Katibu Mkuu wa UN alitangaza kufanyika kwa uchunguzi maalumu ulioongozwa na Katibu Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Taasisi za Sheria na Usalama, Dmitry Titov aliyepewa jukumu la kuchunguza mfululizo wa matukio kadhaa dhidi ya walinda usalama wa UN katika eneo la Beni, jimbo la Kaskazini Kivu, DRC.

Vilevile timu hiyo maalumu ilipewa jukumu la kuchunguza tukio la shambulizi la Desemba 7, mwaka jana ambapo walinda usalama 15 wa Tanzania waliuawa katika kituo chao Semuliki, huku 43 wakijeruhiwa na mmoja mpaka sasa hajulikani alipo. Uchunguzi huo pia umehusisha mashambulizi mawili ya awali dhidi ya walinda usalama wa Tanzania yaliyotokea karibu na Mamundioma Septemba 16 na Oktoba 7, 2017.

“Timu maalumu ya uchunguzi ilikamilisha kwa kusema mashambulizi hayo matatu dhidi ya walinda usalama wa UN yalifanywa kwa modus operandi (njia za uendeshaji) zinazofanana na kwamba ushahidi wote unaonesha ADF kuwa ndio waliofanya mashambulizi,” ilisema sehemu ya ripoti. Ripoti hiyo iliendelea kusema kuwa, “timu hiyo ilibani kuwepo pengo kati ya mafunzo ya MONUSCO na Brigade inayoruhusiwa kupigana (FIB), vilevile Munusco haina mpango mahsusi wa kuongeza nguvu na kuwaondoa walinzi wa amani wakati wakishambuliwa.”

Vile vile ilibaini hakuna amri na udhibiti, ukosefu wa uongozi na wawezeshaji muhimu kama wanaanga, wahandisi na intelijensia navyo ni mapungufu ambayo yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka.
Timu hiyo maalumu ya uchunguzi ambayo inahusisha wataalamu wa wajeshi na usalama, wanasiasa na maofisa wa lojistiki na maofisa wa juu wa Tanzania kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ililenga kutambua mazingira yaliyopelekea mashambulizi hayo, kutathmini hatua za MONUSCO na kubainisha hatua zinazohitajika ili kuzuia mashambulizi zaidi kutokea tena.

Walipendekeza kuwa MONUSCO, Makao Makuu ya UN na majeshi ya nchi zinazoshiriki watafute mikakati yenye kuiwezesha FIB kuwa imara, kuingilia haraka kwenye eneo la vita na kuwa thabiti katika operesheni zinazohitaji nguvu hasa kwenye maeneo ya vijijini na maeneo magumu kufikika. Wachunguzi hao wametaka ushiriki wa wanasiasa wakuu katika ukanda huo na wadau kuelewa na kuchukua hatua dhidi ya vitisho vya ADF.

Kulingana na kile kilichobainishwa na timu hiyo maalumu ya uchunguzi, MONUSCO imeboresha Mpango wa kuboresha Usalama wa Walinda amani ikiwa ni hatua baada ya ripoti ya Jenerali Santos Cruz inayokuwa na mapendekezo kuhusu matukio ya Semuliki na Mamundioma.

Lilikuwa ni shambulizi baya dhidi ya MONUSCO, tangu majeshi ya UN kupelekwa DRC tangu mwaka 1999, na shambulizi baya dhidi ya majeshi ya UN tangu kutokea vifo vya walinda amani 24 kutoka Pakistani waliouawa nchini Somalia mwezi Juni 1993, na kusababisha UN kufanya uchunguzi.
 Akizungumza wakati wa kuaga miili ya wanajeshi waliouawa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliitaka UN kufanya uchunguzi wa tukio hilo. “Serikali ya Tanzania inaomba Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi wa kina, wa wazi na makini… matarajio yetu UN itafanya uchunguzi huo pia haraka,w” alisema.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top