0
WATU watano wakiwemo wanawake wanne na mwanaume mmoja ambaye ni dereva basi ndogo aina ya Toyota Hiache yenye namba za usajili T 962 BSE aliyetambuliwa kwa jina la Jackson Adam wamefariki dunia papo hapo baada yakugongana na basi la New force New lenye namba T 346 DLY likitokea Dar es Salaam – Tunduma na pia kusababisha majeruhi tisa kulazwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Miongoni mwa wanawake ni pamoja na Witness Leonard Mwamuni (26) ambaye watoto wake wawili aliokuwa amesafiri nao kwenye basi dogo hili wamejeruhiwa na kulazwa wodi nne kaika hospitali hiyo.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alithibisha kutokea kwa ajali hiyo majira ya saa nne asubuhi ya Machi 4, mwaka huu katika barabara kuu ya Morogoro – Iringa. Alisema ajali hiyo ilihusisha basi la aina ya Yuntong lenye namba za usajili T 346 DLY mali ya kampuni ya New force New ikitokea Dar es Salaam kwenda Tunduma kugongana na basi ndogo aina ya Toyota Hiache yenye namba za usajili T 962 BSE ikitokea Kata ya Mlali, wilaya ya Mvomero kwenda Morogoro Mjini.
Kamanda Matei alisema ,katika ajali hiyo , abiria watano walikuwa ndani ya Toyota Hiache walifariki dunia papo hapo na tisa kujeruhiwa na kukimbizwa hospitali ya Rufaa ya Morogoro kupatiwa matibabu. Kamanda wa Polisi wa mkoa huyo aliwataja , waliofariki dunia ni dereva wa basi dogo Jackson Adam ambaye ni mkazi wa Kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro, Georgina Aloyce (35) , Revocatha Raymond Lyimo , Mangasa Almasi na Witness Leonard Mwamuni (26).
Pia aliwataja majeruhi wa ajali hiyo wote kutoka basi dogo ni watoto wawili waliofiwa na mama yao katika ajali hiyo, Catharine Mhagama (6) na Caltimei Mhangama mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili ( 1.1/2) , Prisca Isaya (25). Wengine ni Chuki Wage (40), Anthon Cletus Mhando (39) mkazi wa eneo la SUA, Innocent Emilian , Willborod Emilian ambao ni watu wazima mapacha , Iman Amri Salum pamoja na kondaka wa daladala hiyo Ally Ramadhan.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi huyo kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi dogo ambaye ni marehemu kutaka kulipita lori la mchanga lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na hivyo kwenda kugonaga na basi la Kampuni ya New Force ambalo lilikuwa likiendeshwa na Mduika Manyema (52) mkazi wa Dar es Salaam.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top