0
MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk Jim Yonazi ametoa rai kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kushirikiana na vyombo vya serikali katika kuhakikisha habari zinawafikia wananchi sanjari na kutangazwa kwa habari za mkoa huo.
Dk Yonazi aliyasema hayo wakati alipofika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kwa ajili ya kujitambulisha na kubadilishana uzoefu.
Alisema, vyombo vya serikali vinapaswa kutangaza habari za serikali na nyinginezo, hivyo ni vyema wanahabari wa serikali wakapewa ushirikiano ili kuwezesha habari mbalimbali, kuwafikia wananchi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Alisema, kila mkoa una mambo yanayopaswa kutangazwa, hivyo ni vyema uongozi wa mkoa huo ukashirikiana na waandishi wa habari wa magazeti ya serikali ya HabariLeo na Daily News kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii.
“Tunaomba ushirikiano kati yetu na ofisi yako ili kuhabarisha umma mambo mbalimbali yanayohusu Mkoa wa Arusha,” alisema Dk Yonazi.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo alisema kuwa ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa magazeti ya serikali na vyombo vingine vilivyopo mkoani humo kwa lengo la kutoa habari kwa umma kuhusu shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Mkoa.
Katika ziara hiyo, Dk Yonazi pia alikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega na kufanya mazungumzo na wafanyakazi wa TSN mkoani hapo katika ofisi zake zilizopo jengo la Kibla Complex kuhusu uboreshaji utendaji kazi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top