0
Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakitafanya mazungumzo kusaka suluhu na mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba, kipo tayari kwa lolote hata kama kitafutiwa usajili.
 
Aidha, chama hicho kimesema hakijutii kumkaribisha na kumuunga mkono Edward Lowassa, ambaye aliteuliwa kugombea urais mwaka 2015 kwa tiketi ya Chadema na kuwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
 
Hayo yamesemwa na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF,  Mbarala Maharagande kujibu madai yaliyotolewa na Profesa Lipumba alipokuwa akifanya mahojiano na kituo kimoja cha televisheni hapa nchini.
 
Katika mahojiano hayo, Profesa Lipumba alidai kuwa mgogoro uliopo ndani ya chama hicho kwa sasa hautamalizwa na mahakama pekee bali viongozi wa pande zote mbili wanatakiwa kuzungumza, lakini Maharagande amesema haiwezekani kwa vile Lipumba alishakwisha kukivuruga chama na hafai tena kuendelea kuwa kiongozi.
 
“Lipumba anasema tukae tulimalize suala hili kwa kuongea sisi wenyewe. Jambo hilo haliwezekani kwa kuwa kama kupandikiza chuki, uhasama, uharibifu wa chama miongoni mwa wanachama na viongozi ameshafanya na kufanikiwa hilo kwa baadhi ya wanachama na viongozi wake na kuharibu taswira ya chama kwa jamii,” amesema Maharagande.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top