Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip
Isdor Mpango (Mb) katika Mkutano na Sekta Binafsi nchini (TPSF), Jijini Dar es
Salaam.
Waziri Mpango amesema kuwa ni vema Sekta Binafsi ikashirikiana na
Sekta ya Umma kwa kuwa zote zinategemeana na hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa
na Sekta Binafsi ambayo ni imara.
“Sekta Binafsi na Sekta ya Umma hazina budi kufanya kazi kwa
kushirikiana kwa karibu, tena kwa kuaminiana kwa faida ya Sekta zote mbili na
kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla” aliongeza Dkt. Mpango.
Amesema kuwa, lengo la pande zote mbili ni kuharakisha utekelezaji
wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza fursa za ajira, kipato cha
mwananchi na kuondokana na umasikini uliokithiri kwa kujenga Tanzania
inayoongozwa na uchumi wa Viwanda.
Dkt. Mpango alifafanua kuwa Serikali imeendelea kuyafanyia kazi
mapendekezo mengi yaliyotolewa na Sekta Binafsi ikiwemo katika kuboresha
mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwa
wafanyabiashara.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na
Serikali kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa
Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha mamlaka ya kusamehe Kodi ya Ongezeko
la Thamani bila kuhusisha utaratibu wa kulipa kwanza Kodi ya Ongezeko la
Thamani na baadaye kuomba kurejeshewa (Refund) kwenye miradi inayofadhiliwa na
wadau wa maendeleo (Grants) au mikopo yenye masharti nafuu (Concessional Loans)
ambayo mikataba husika ina masharti ya kutoa msamaha wa kodi hiyo.
“Hatua hii itawezesha wakandarasi wanaotekeleza
miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kutopata tena usumbufu katika kutekeleza
miradi hiyo na miradi kutekelezwa kwa muda uliopangwa” alisema Dkt. Mpango
Ili kuvutia uwekezaji katika sekta za viwanda,
kilimo cha mazao na mifugo nchini, Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwenye bidhaa za mtaji (capital goods) za viwanda vya mafuta ya kula,
nguo, ngozi, madawa ya binadamu na mifugo ili kupunguza gharama za
ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo watakayonunua wawekezaji kwa ajili ya
kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
“Serikali sasa inatoza Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwa kiwango cha asilimia sifuri katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji
wa bidhaa/mizigo nje ya nchi (ancillary transport services), hatua itayopunguza
gharama za usafirishaji katika bandari zetu na kuifanya Tanzania kuwa njia bora
zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine hususan
zisizo na bandari.
Kwa upande wa hali ya Uchumi, Waziri Mpango amesema kuwa robo ya
kwanza ya mwaka 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ulikua kwa
asilimia 7.8, hivyo kufanya nusu ya kwanza uchumi kukua kwa asilimia 6.8.
Baadhi ya shughuli za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi ni usafirishaji
na uhifadhi wa mizigo ambao umekua kwa asilimia 19.8, uchimbaji madini na mawe
asilimia 18.0, uzalishaji viwandani asilimia 9.3 na ujenzi asilimia 8.8.
Dkt. Mpango alisema Sekta ya Benki kwa ujumla imeendelea kuwa
imara ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha juu ya viwango vinavyokubalika
kisheria. Kwa kipindi cha mwaka 2009
hadi 2017 huduma jumuishi za fedha zimeongezeka kutoka asilimia 15.8 hadi asilimia 65.3. Upatikanaji
wa huduma za kifedha umeongezeka kutoka asilimia 29 kwa mwaka 2009 hadi
asilimia 86 kwa mwaka 2017.
Aidha kwa upande wa mikopo kwa Sekta Binafsi ilipungua kutokana na
Benki kuchukua tahadhari kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu (Non-performing
loans) ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua kwa kupunguza kiwango
cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki Kuu kama dhamana
kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 na riba za mikopo ya benki hizo kushuka kutoka
asilimia 16 hadi 12.
Naye mwenyekiti mwenza wa Mkutano huo Waziri wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (Mb) amesema kuwa njia bora ya kutatua
matatizo ya Sekta Binafsi ni kuendelea kufanyika kwa majadiliano yenye tija.
Mmoja wa wajumbe wa Mkutano huo wa wafanyabiashara ambaye ni
wakili wa kujitegemea Bi. Eve Hawa Sinare amesema kuwa ni vema kuangalia mfumo
mzuri wa kuweka riba unaofanywa na Benki za biashara ili kuwa na uwiano mzuri.
Vilevile Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Bw. Salum
Shamte ameishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya dhati ya kushirikiana na Sekta
hiyo kwa lengo la kufanikisha ukuaji wa uchiumi wa Viwanda.
Waziri mpango amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali
itaendelea kuhakikisha kuna majadiliano ya mara kwa mara na wadau hao ili
kutatua changamoto zao na pia ameahidi kuandaa Mkutano mwingine ambao utajikita
katika masuala ya kodi kabla ya Sekta Binafsi kuwasilisha mapendekezo ya kodi.
Mkutano huo wa Sekta Binafsi na Umma ni wa pili kufanyika, kwa
mara ya kwanza Mkutano kama huo ulifanyika tarehe 11 Aprili, 2017 mjini Dodoma
ambapo ulisaidia kutatua changamoto
nyingi ikiwemo kusaidia kuongezeka kwa ufanisi katika huduma za bandari nchini.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na
Mipango
Post a Comment
karibu kwa maoni