0
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert BoazMKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz amesema Jeshi la Polisi bado linaendelea na upelelezi juu ya tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Amesema matukio mengine, ambayo jeshi hilo linayafanyia kazi kwa nguvu zote ni suala la kupotea kwa aliyekuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane na tukio la kutoweka kwa Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea wa gazeti la Mwananchi mkoani Pwani, Azory Gwanda. DCI Boaz alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama nchini.
Akizungumzia tukio la Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu, Boaz alisema jeshi hilo lilizingatia suala hilo kwa ukaribu na wanachukua hatua zote ili kubaini nani alihusika katika kutenda tukio hilo.
“Suala hili limezungumzwa sana na viongozi, nisingependa kulizungumzia sana hapa, lakini niwahakikishie kwamba Jeshi la Polisi linachukulia tukio hilo seriously, sisi hatuwezi kujibizana na watu kwenye magazeti, bali tunachukua hatua zote ambazo zinatuwezesha kutambua nani amehusika na tukio hili,” alisema.
Kuhusu Saanane ambaye amefikisha mwaka mmoja tangu kupotea kwake, alisema wameshachukua kila hatua inayostahili kufanywa na kuwataka wananchi wenye taarifa kuhusu tukio hilo, wapeleke taarifa polisi.
“Tumeshalisema sana suala hili, sisi kama wapelelezi hatuwezi kusema kila hatua tunazochukua, hairuhusiwi kisheria, hairuhusiwi katika kanuni zetu za upelelezi. Lakini niwahakikishie kwamba kila hatua ambayo inastahili kufanywa kuweza kumfuatilia mtu imeshafanyika.
Nitoe rai kwenu na wananchi kwamba wale ambao mna taarifa mtuletee,” alisema Boaz. Kwa upande wa mwandishi Gwanda, ambaye amemaliza mwezi mmoja tangu apotee, Boaz alisema wamepokea taarifa za kupotea kwake na kwa taratibu za jeshi hilo, wanachukua kila hatua inayostahili kuchukua wakati wa kumtafuta mtu aliyepotea, kwa kuwa ziko taratibu ambazo zinapaswa kuchukuliwa kama polisi, hivyo jamii iwe na subira wakati wanaendelea na upelelezi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top