0
Uvutaji wa shisha umepigwa marufuku nchini Tanzania, Rwanda na Kenya.KENYA imeungana na Tanzania na Rwanda, kupiga marufuku uingizaji, uuzaji na matumizi ya tumbaku, inayovutwa kwa kutumia chombo maalumu cha kutolea moshi, ambacho huwekwa tumbaku, maji na moto na kisha mtumiaji kuvuta, mara nyingi na zaidi ya mtu mmoja.
Ni aina ya ulevi ulioibuka kwa kasi na kuteka vijana wengi, walioigeuza kuwa starehe au anasa mpya katika sehemu mbalimbali za mijini. Uamuzi wa Serikali ya Kenya ulitangazwa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Dk Cleopa Mailu akisema watakaokiuka agizo hilo, watakumbana na faini ya hadi Shilingi 50,000 za Kenya, sawa na Dola za Marekani 500 au kifungo cha hadi miezi jela, au adhabu zote kwa pamoja.
Aidha, kwa watakaokutwa wakijihusisha na Shisha, kwa namna moja ama nyingine, watakabiliwa na faini ya dola 10 kila siku ambayo mtu atafanya kosa. “Hakuna kuingia, kuzalisha, kuuza, kutumia, kutangaza au kuishabikia kwa namna yoyote ile ndani ya Kenya.
Ni marufuku,” alisema Dk Mailu. Kenya inakuwa nchi ya tatu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yenye nchi sita kupiga marufuku shisha. Zilizotangulia kupiga marufuku ni Tanzania na Rwanda, Nchi nyingine za EAC ni Burundi, Uganda na Sudan Kusini.
Nje ya Afrika, nchi nyingine zilizopiga marufuku matumizi ya shisha ni Pakistan, Jordan, Singapore na Saudi Arabia. Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Kenya, Jackson Kioko alisema: “Uamuzi wetu wa kupiga marufuku matumizi ya shisha unalenga kulinda afya za raia kwa sabau uvutaji wake una madhara kiafya.”
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mkupuo mmoja wa shisha una kemikali hai 4,800 na kwamba kemikali hizo husababisha saratani ya mapafu, maradhi ya moyo na matatizo katika mfumo wa hewa. Taarifa hizo za WHO zinaeleza kwamba, kiasi cha uvutaji wa shisha kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara kati ya 100 na 200.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top