0

Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) kesho linatarajiwa kutoa tuzo za mchezaji bora wa Afrika mwaka 2017. Tuzo hizo zitafanyika jijini Accra nchini Ghana ambapo mchezaji mmoja kati ya watatu waliofika fainali atatangazwa mfalme.
Wachezaji watatu waliotajwa katika orodha ya mwisho ni mshindi wa tuzo hiyo mwaka 2015 Pierre-Emerick Aubameyang raia wa Gabon ambaye anacheza klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani. Wengine ni Sadio Mane wa Senegal na Liverpool pamoja na Mohamed Salah wa Misri na Liverpool.
Aubameyang mwenye umri wa miaka 28 aliibuka kinara wa mabao katika ligi kuu ya Ujerumani baada ya kufunga mabao 31 katika mechi 32 alizocheza. Hapewi nafasi kubwa sana ya kushinda kutokana na kushindwa kutoa mchango kwenye timu yake ya taifa ya Gabon ambayo haikufanya vizuri kwenye michuano ya AFCON 2017 iliyofanyika nchini kwao.
Sadio Mane ameisaidia timu yake ya Senegal kutinga kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 ndhini Urusi, hivyo anapewa nafasi ya kushinda. Nyota wa Liverpool na Misri Mohamed Salah anaongoza kwa kupewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo baada ya kuisaidia Misri kufuzu Kombe la Dunia baada ya miaka 25 kupita.

Salah pia amekuwa kwenye kiwango kizuri msimu huu baada ya kutua Liverpool akitokea Roma ya italia. Hadi sasa Salah anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji kwenye EPL akiwa na mabao 17.
Mshindi wa tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wa ndani mwaka 2015, Mbwana Samatta anayechezea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji alitajwa kwenye orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo hii lakini aliondolewa kwenye mchujo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top