ZAIDI ya wakazi elfu 16 wa vijiji vitatu vya Mauno, Makiranya na Kinyasi-Majengo, katika Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma wameondokana na adha ya kukosa maji baada ya kuzinduliwa kwa visima viatu vya maji vilivyojengwa kwa msaada wa wahisani kutoka nchini Uturuki kupitia ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa visima hivyo
katika Kijiji cha Mauno, Kata ya Bumbuta, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dokta Ashatu Kijaji, amesema
kuwa kuzinduliwa kwa visima hivyo kunalifanya jimbo lake lifikishe visima 41
hatua ambayo amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika jimbo
lake.
Dkt. Kijaji ameushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa kuratibu
msaada huo wa zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 36, sawa na shilingi milioni 81,
zilizotumika kuchimba visima hivyo pamoja na kuweka miundombinu mingine
zikiwemo jenereta zinazotumika kusukuma maji hayo na kuwezesha upatikanaji wa
maji hayo.
“Hivi sasa ujenzi wa visima 15 kati ya 25 vinavyojengwa na
Serikali kupitia Wizara ya Maji unaendelea huku wahisani wakiwa wametujengea
visima 36 hivyo kufikisha idadi ya visima 61 katika kipindi cha miaka miwili tu
tangu Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
aingie madarakani hali ambayo haijawahi kutokea na lengo letu ni kuhakikisha
kuwa vijiji vyote 84 vinapatiwa huduma ya maji ifikapo mwaka 2020” Alisisitiza
Dkt. Kijaji
Diwani wa Kata ya Bunbuta Bw. Bashiru Mtolo na mkazi mmoja
wa kijiji hicho Bi. Khadija Hussein wamesema kuwa tatizo la maji katika kijiji
cha Mauno lilikuwa kubwa na kuwalazimisha wanawake na watoto kwenda umbali
mrefu kusaka maji kwa ajili ya matumizi yao ya majumbani pamoja na kunywesha
mifugo.
“Tunaushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa msaada wao huu mkubwa
na Mbunge wetu kwa ufuatiliaji wake wa karibu uliowezesha kupatikana kwa visima
hivi na vingine ambavyo vimesaidia kwa kiwango kikubwa kutatua kero ya maji na
tunaamini mpaka kufikia mwaka 2020, matatizo ya maji katika wilaya yetu ya
Kondoa litakuwa historia” alisema Diwani Mtolo.
Naye Mwakilishi na Mwambata wa Ubalozi wa Uturuki hapa
nchini Sheikh Muhammad Cicek ameeleza kuwa msaada wa Dola elfu 36 zilizotumika
kujenga miradi hiyo mitatu ya visima vya maji umetolewa na wahisani mbalimbali
wa Uturuki ikiwa ni kuenzi uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na Tanzania.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo ya maji kutasadia
kuwawezesha akina mama na wananchi wa Kondoa kwa ujumla kufanya shughuli
nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji ambayo hata
hivyo hayakuwa safi wala salama.
Post a Comment
karibu kwa maoni