
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amewataka madiwani wa vyama vya
upinzani kujiunga na CCM ili waweze kushirikiana naye kutekeleza ilani
ya uchaguzi ya chama tawala.
Amesema
yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa
manane, ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.
Akizungumza
jana Februari 11, 2018 katika mkutano wa hadhara kata ya Haydom
wilayani Mbulu, Mnyeti amesema ni vyema madiwani wa Chadema wakajiunga
na CCM.
Amesema
diwani wa Chadema ni ngumu kufanikisha maendeleo ya wananchi kwa madai
kuwa, hakuna ambaye atamsikiliza akiwasilisha hoja zake katika vikao vya
halmashauri husika.
"Hata
hapa Haydom najua ni ngome ya Chadema hata mwenyekiti wa kijiji namuona
ana damu ya CCM, sasa ondokeni huko mje huku tutekeleze ilani ya
uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa kuleta maendeleo," amesema Mnyeti.
Awali,
mkazi wa kata ya Hayderer, John Tluway aliuliza swali kwa mkuu huyo wa
mkoa akitaka kujua sababu za mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga
kutofika kwenye kata hiyo inayoongozwa na Chadema.
Akijibu
swali hilo, Mnyeti amempongeza Mofuga kwa kutokufika kwenye kata hiyo
inayoongozwa na Chadema kwa maelezo kuwa diwani wa kata hiyo anapaswa
kujiunga na CCM ili kufanikisha maendeleo.
"Mkuu
wa wilaya ninakupongeza kwa wewe kutofika kwenye kata hiyo kwani
ningepata taarifa umefika mara ya kwanza, mara ya pili na mara ya tatu
ningekuwa na mashaka na wewe lakini hongera sana kwa kutokwenda," amesema Mnyeti.
Pia,
amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kutekeleza na kufanikisha kwa
vitendo ilani ya CCM hata kama hawana kadi ya chama hicho kwani ndicho
ambacho kipo madarakani.
"Mtekeleze
hayo kwa nia safi, hiyo ni sawa na imani kwani hata kanisani huwezi
kusikia padri akimsifu Muhammad na pia kule msikitini imamu huwa hamsifu
Yesu," amesema Mnyeti.
Mwenyekiti
wa CCM wa Wilaya ya Mbulu, Nasaeli Sulle alimhakikishia Mnyeti kuwa
wananchi wa Haydom wamejitambua kuwa walifanya makosa na kuchagua
Chadema ila sasa wapo tayari kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM.
Post a Comment
karibu kwa maoni