
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata na kutaifisha bidhaa mbalimbali
ikiwa ni pamoja na tani moja ya sukari na chumvi, majani ya chai mifuko
18, mirungi kilogramu 16, vifaranga vya kuku 5000 na mayai kasha 416
katika mpaka wa Namanga mkoani Arusha zikitokea nchini Kenya kupitia
njia zisizo rasmi.
Akizungumza
mara baada ya kukamata bidhaa hizo, Meneja Msaidizi wa Forodha mkoani
hapo Edwin Iwato alisema bidhaa hizo ni mali ya Joseph Sekino, Innocent
Minja na Andrew Lyimo wote wakiwa ni wafanyabiashara kutokea Tanzania na
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
“Tumewakamata
wafanyabiashara watatu ambao ni Joseph Sekino akiwa amepakia tani moja
ya sukari na chumvi na majani ya chai mifuko 18 kwenye gari Na. T 785
AWV, Innocent Minja akiwa na mayai kasha 416 na mirungi kilo 16 kwenye
gari Na. T 443 CQU na Andrew Lymo akiwa na vifaranga vya kuku 5000
kwenye gari Na. T 441 DHW wote wakitokea nchini Kenya kuja mkoani
Arusha,” alisema Iwato.
Iwato
alieleza kwamba, wafanyabiashara hao waliingiza baadhi ya bidhaa hizo
kwa kutumia vifungashio vya bidhaa nyingine za nchini Tanzania ili
kuficha uhalisia wake huku wakiwa hawana vibali wala kulipa ushuru wa
Serikali kama inavyotakiwa.
Alifafanua
kuwa, mirungi ilikamatwa ndani ya mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo
ikiwa imefichwa kwenye boneti ya mbele ya gari aina Noah Na. T 443 CQU
sehemu ya injini.
Naye,
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Richard Kayombo
alisema, tabia ya wafanyabiashara hao siyo tu inawahujumu
wafanyabiashara wenzao bali inakwamisha azma ya Serikali ya kukusanya
mapato kwa ajili ya maendeleo ya kila mwananchi.
“Tabia
ya wafanyabiashara hawa siyo nzuri kwa kuwa inakwamisha ukusanyaji
mapato ya Serikali na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili
iwe fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya biashara pasipo kutumia
njia rasmi na kulipa ushuru ipasavyo”, alisema Kayombo.
Aidha,
Kayombo aliongeza kuwa, bidhaa zote haramu zilizokamatwa zitateketezwa
kwa mujibu wa Sheria, zile zinazofaa kwa matumizi ya binadamu zitagawiwa
kwa taasisi mbalimbali za Serikali zenye uhitaji kwa mujibu na taratibu
zilizowekwa na TRA na magari yote yaliyotumika kusafirisha bidhaa hizo
yametaifishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Utaifishaji
wa magari na bidhaa ambao usafirishaji wake haufuati sheria na
taratibu, unalenga kukomesha shughuli za magendo nchini ambazo kwa kiasi
kikubwa zinakwamisha juhudi za Serikali katika ukusanyaji wa mapato.
Post a Comment
karibu kwa maoni