Uamuzi wa Serikali wa kupunguza kiwango cha
chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na benki za
biashara nchini, umechochea taasisi za
fedha yakiwemo mabenki kuanza kupunguza viwango vya riba ya mikopo hatua
itakayochochea ukuaji wa uchumi.
Hayo yalisemwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kufunga warsha ya
wadau wa Sekta ya Fedha uliowashirikisha wabunge, washirika wa Maendeleo, wakuu
wa Taasisi za fedha na Wizara ya Fedha na Mipango.
Dkt. Kijaji, alisema kuwa Serikali kupitia Benki Kuu imeshusha riba ya mikopo
kwa taasisi za fedha kutoka asilimia 16.0 hadi
asilimia 9.0 na kupunguza kiwango
cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa katika Benki hiyo na benki za
biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0
kuanzia mwezi Aprili 2017, jambo ambalo limeleta matokeo
chanya katika kuimarisha uwezo wa taasisi kukopesha wateja wao.
Miongoni mwa Benki zilizoshusha viwango vyao vya riba za mikopo ni CRDB ambayo
imetangaza kushusha riba kutoka asilimia 22 hadi 16 na kuongeza kiasi cha
kukopa kwa wafanyakazi kutoka Sh. milioni 50 hadi Sh. milioni 100 huku muda wa kurejesha
ukiongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.
Benki nyingine ni NMB ambayo imeongeza muda wa
marejesho ya mikopo kwa wafanyakazi, wajasiriamali wadogo na wakubwa kutoka
miezi 60 hadi 72, na imepunguza riba ya
mikopo kwa wafanyakazi kutoka asilimia 21 hadi 19 na wajasiriamali wadogo
kutoka asilimia 23 hadi 21.
Dkt.
Kijaji amezipongeza benki zilizoshusha viwango vya riba na ameitaja
hatua hiyo kuwa ni muhimu katika kuifikisha Tanzania kuwa nchi
ya viwanda hata kabla ya mwaka 2025 na kutoa wito kwa taasisi hizo za
fedha
kuitupia jicho sekta ya kilimo kutokana na umuhimu wake katika kutimiza
malengo
ya kukuza viwanda.
Aidha,
Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imekamilisha andiko “Blue Print” ambalo lengo
lake ni kuboresha mazingira ya kufanya
biashara nchini ili kuleta tija kwa wafanyabiashara na Sekta ya Fedha kwa
ujumla
Alisema Serikali imeendelea
kulipa malimbikizo ya madai mbalimbali yaliyohakikiwa ya watumishi, wakandarasi
na watoa huduma wengine yaliyohakikiwa ili
kuongeza ukwasi katika jamii na kwa kwamba uhakiki uliofanyika umeokoa kiasi
kikubwa cha fedha za Serikali ambazo zingelipwa wakati madai hayakuwa sahihi.
Naibu Waziri huyo aliipongeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kushiriki kwa
vitengo katika utekelezaji wa Mpango huo kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya
kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo la Mkulazi na Mbigiri -
Morogoro na mradi wa ujenzi wa machinjio
ya kisasa ya nyama eneo la Makunganya
mkoani humo.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu,
alieleza kuwa warsha hiyo iikuwa na manufaa makubwa na kwamba Wizara inaandaa
mkakati wa utekelezaji wa Sekta ya Fedha wa Miaka kumi ambao utakujumuisha pia
mawazo ya wadau hao.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. Honest Ngowi, amepongeza hatua ya Serikali ya kuwa na
majadiliano na Sekta ya fedha kwa kuwa ina mchango mkubwa katika kutekeleza
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Akitoa tathimini yake kuhusu utekelezaji wa Mpango huo, Prof. Ngowi,
alisema kuwa sehemu ya miradi kumi ya kipaumbele, ikiwemo ujenzi wa Reli ya
Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ufufuaji wa Shirika la Ndege na Ujenzi wa
Kiwanda cha Sukari Mkulazi mkoani Morogoro, ni baadhi ya miradi muhimu
inayotekelezwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni