Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza kuanza
kupokea maombi ya mwaka wa masomo 2018/19 kuanzia leo hadi Julai 15,
mwaka huu.
Taarifa
iliyotolewa katika mtandao wa kompyuta wa HESLB jana ilieleza kuwa
maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao ambao umefanyiwa maboresho
na Kituo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UCC-UDSM).
"Tunawataarifu
watarajiwa wanufaika wa mkopo wapya na wa zamani kwa mwaka 2018/19 kuwa
mfumo wetu wa maombi kwa njia ya mtandao utafunguliwa kuanzia Alhamisi
Mei, 10 (leo) hadi Jumapili Julai 15, 2018," ilieleza taarifa hiyo.
Kadhalika,
HESLB iliwataka wanufaika na watarajiwa wa mkopo kuzingatia mwongozo wa
utoaji mkopo na ruzuku kwa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2018/19.
Sehemu
ya maelezo ya mwongozo wa utoaji mkopo inasema waombaji wote
wanakumbushwa kuhakikisha maelezo wanayoyatoa katika fomu ya maombi ya
mkopo, yawe sawa na maombi ya udahili wa chuo.
Pia ilieleza kuwa namba ya mtihani wa kidato cha nne iwe sawa na iliyopo kwenye maombi ya mkopo na udahili wa chuo.
Kadhalika, bodi imewataka waombaji kuhakikisha nyaraka zote za maombi ya mkopo wanazowasilisha zimehakikiwa na mamlaka husika.
HESLB
imetaka waombaji kuhakikisha vyeti vyote vya kuzaliwa na vifo na
vingine vinathibitishwa na Mamlaka ya Vizazi na Vifo (RITA) au ofisa
aliyechaguliwa, ili kuthibitisha uhalali huo.
"Hata
hivyo, Ofisa Wilaya Ustawi wa Jamii (DSWO) anaweza kuidhinisha ripoti
ya kifo cha mzazi kutoka kwa mamlaka ya kijiji au kata," ilisema taarifa
hiyo.
Mwongozo
huo pia uliwataka waombaji kuhakikisha taarifa kuhusu wazazi, walezi na
mdhamini (kazi, anuani ya mwajiri, namba ya simu, anuani ya posta) ziwe
kamili na sahihi.
"Waombaji
mikopo ambao wazazi wao ni viongozi waliotajwa katika Kanuni ya Uongozi
wa Umma, hawapaswi kuomba kwa Sheria ya Mwaka 1995," taarifa ilifafanua
na kueleza zaidi:
"Vilevile
waombaji ambao wazazi au walezi ni wamiliki wa biashara, mameneja
wakubwa katika mamlaka zinazotambulika zenye usajili, hawaruhusiwi
kuomba mkopo."
Sehemu
ya mwongozi huo inawataka waombaji kukamilisha fomu zao kwa usahihi na
mara wanapowasilisha hawataweza kurekebisha taarifa hizo iwapo
huwakujaza kwa ufasaha.
Pia
iliwataka waombaji kutunza nakala za maombi ya mkopo waliyowasilisha
HESLB kwa matumizi mengine endapo itahitajika, pamoja na kuzingatia muda
wa kutuma maombi.
Aprili
17, HESLB ilitangaza kuanza kupokea maombi kwa mwaka wa masomo 2018/19
kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi huu.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na bodi hiyo, mikopo hiyo
ilikuwa ikisubiri maboresho ya mfumo wa uombaji mikopo kwa njia ya
mtandao.
Katika
taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema
maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao wa www.olas.heslb.go.tz.
Katika
taarifa hiyo, Badru alisema kwa uzoefu wa miaka iliyopita waombaji wa
mikopo waliwasilisha maombi yao bila kuzingatia mwongozo uliotolewa na
kusababisha baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo.
"Mwaka
jana (2017), kwa mfano, zaidi ya waombaji 10,027 kati ya waombaji zaidi
ya 61,000 hawakuambatanisha nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au
hata vile vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA) kama tulivyoelekeza," alisema.
Alitaja
nyaraka nyingine muhimu ambazo waombaji mikopo wanapaswa kuziandaa ni
pamoja na nakala za vyeti vya kitaaluma za kidato cha nne, sita na
stashahada ambazo zimethibitishwa na Kamishna wa Viapo - yaani wakili au
hakimu.
Aidha,
Badru alisema wanafunzi waombaji wenye ulemavu au wenye wazazi wenye
ulemavu wanapaswa kuwa na barua zinazothibitisha ulemavu huo kutoka kwa
Mganga Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Kituo cha Afya cha Serikali.
Pia
alisema wanafunzi ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya sekondari au
stashahada (diploma) wawe na barua za uthibitisho wa udhamini huo
kutoka katika taasisi zilizogharamia masomo yao.
Post a Comment
karibu kwa maoni