Serikali
imesema tayari nchi imeanza rasmi majaribio ya dawa kinga mpya
inayozuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi (PrEP), huku ikikanusha kuwapo
kwa dawa inayotibu ugonjwa huo.
Dawa
kinga hiyo mpya ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
(VVU) ikiwa mtumiaji atameza kila siku kwa muda wa siku saba kabla
hajashiriki tendo la kujamiiana, ataendelea kumeza kwa kipindi chote
atakachokuwa katika hatari ya kuambukizwa.
Hayo
yamesemwa leo Mei 9, 2018 mjini Dodoma na naibu waziri wa Afya, Dk
Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa mpango wa nne wa VVU na Ukimwi
katika sekta ya afya (HSHSP IV 2017-2022) sambamba na maadhimisho ya
miaka 30 ya Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi.
Amesema taarifa kwamba nchi inazindua tiba dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, si sahihi kwani Tanzania haijapata tiba hiyo.
"Kinachoendelea
tumezindua dawa kinga, kuna dawa ambayo tunataka tuielekeze katika
makundi ambayo tunayaona yapo kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya
Ukimwi, watapatiwa kwa lengo la kuwakinga wasipate,” amesema Dk
Ndugulile na kuongeza:
“ila
sio suluhisho na tuseme vilevile kwamba hatujapata tiba ya virusi vya
Ukimwi na utaratibu huu wa dawa kinga, ndiyo inaanza majaribio sasa na
haijaanza kupatikana.”
Dawa
hizo mpya zenye uwezo wa kukinga maambukizi dhidi ya VVU kwa asilimia
99, zilizoanza kutumika katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika,
zinakuja wakati ukanda huo ukiongoza duniani kwa kuwa na asilimia 50 ya
waathirika wote duniani.
Utafiti
uliofanywa na mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha London, Dk Sheena
McCormack umeonyesha kuwa PrEP inazuia maambukizi ya Ukimwi kwa kuua
virusi baada ya kufanyiwa majaribio na kundi la wapenzi wa jinsia moja,
ambao wamo katika hatari zaidi ya maambukizi.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetambua kwamba dawa hiyo ya tembe inaweza kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa.
Post a Comment
karibu kwa maoni