0
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeitaja Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zenye matumizi bora ya fedha zinazofadhiliwa na Benki hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya miundombinu ya barabara na nishati.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayesimamia nchi 7 za Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro wakati  wa kikao  cha Magavana wa nchi za Afrika kwenye Mkutano wa  mwaka wa Benki ya AfDB unaoendelea Mjini Busan, Jamhuri ya Korea ya Kusini.
Dkt. Nyamajeje alisema kuwa changamoto nyingi zinazotokea katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa nchi  za Afrika zinatokana na  ukosefu wa  wataalamu wa fani mbalimbali, jambo linalosababisha miradi mingi  kutomalizika kwa wakati  hata hivyo Benki ya AfDB inaendelea kuangalia ni jinsi gani inaweza kusaidia kutatua matatizo hayo na kuleta maendeleo chanya kwa nchi za Afrika.
Akizungumza katika Mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Amina Khamis Shaaban, alisema kuwa Serikali ya Tanzania imesawasilisha barua kwa uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, ili iweze kusaidia katika ujenzi wa  Uwanja wa ndege ya Msalato Jijini Dodoma na Uwanja wa ndege wa Zanzibar,  aidha miradi hiyo ikiridhiwa na kutekelezwa  itakua kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa Viwanda nchini Tanzania.
Tanzania ni wadau wakubwa  katika Benki ya AfDB hivyo inanufaika na mikopo nafuu inayotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile ujenzi wa Barabara  za kiwango cha Lami hususani mkoa wa Tabora na pia miradi ya  Nishati  ya umeme na maji maeneo mbalimbali nchini.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top