0


JUMLA ya vituo 710 vya mafuta vilifungwa nchi nzima tangu ianze kazi ya kuvikagua vituo hivyo kuona kama vinatumia mashine za kieletroniki za malipo (EFDs).
Vituo 469 kati ya hivyo vimefunguliwa baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na Mamlala ya Mapato Tanzania (TRA) ambavyo ni kulipia gharama za ufungaji mashine hizo kwa mawakala walioidhinishwa na TRA kisha kuingia makubaliano ya muda maalumu wa kuhakikisha kuwa mashine hizo zimefungwa.
Kigezo kingine ni kufunga mashine za EFPP kwa wale wote waliokwishanunua, lakini hawakufunga au waliofunga mashine hizo, lakini wakawa hawajaunganisha na pampu zao za mafuta. Vituo vingine 241 havijafunguliwa kutokana na kushindwa kukidhi masharti ya TRA.Kwa mujibu wa Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya, makubaliano hayo ya muda maalumu yanamruhusu mmiliki wa kituo cha mafuta kuendelea kutumia mashine za kawaida mpaka hapo mashine za kisasa zitakapofungwa.
Aidha, Kamishna Mwandumbya alisema wamiliki wa vituo vya mafuta ambao watashindwa kutekeleza agizo la kufunga mashine za malipo za kielektroniki za kutolea risiti kwa muda uliowekwa watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungwa vitu vyao na kufikishwa mahakamani. Alisema muda waliopewa kufunga mashine hizo hautaongezwa na wamiliki wanapaswa kulizingatia hilo ili kuepuka adhabu, na kwamba baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo wamekuwa siyo waaminifu kwa kuzificha mashine hizo ndani badala ya kuzifunga kwenye pampu na wengine wamezifunga, lakini hawakuziunganisha na pampu.
Aliongeza kuwa wamiliki wa vituo vya mafuta wanatakiwa kuwasiliana na mawakala wa usambazaji wa mashine za kielektroniki na kueleza mahitaji yao ili wajulishwe gharama za mashine na gharama za kuzifunga. Alisema kuna jumla ya mawakala tisa waliopewa jukumu la kusambaza mashine hizo nchini na kuwataja baadhi yao kuwa ni Advatech Technologies Ltd, Pergamon Ltd na Web Technologies Ltd.
Mwandumbya alisema asilimia 70 ya vituo vya mafuta nchini vinamilikiwa na kuendeshwa na wajasiriamali wadogo wanaojulikana kama DODO (Dealer Owned Dealer Operated). Alisema wafanyabiashara hao kupitia chama chao cha TAPSOA wanamiliki vituo vya mafuta kati ya 1,500 hadi 1,800 nchi nzima.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top