
Waziri
wa Nishati, Medard Kalemani amemtaka Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Abdallah Ikwasa kumuondoa mara moja
meneja uendeshaji wa kituo cha umeme Kidatu akituhumiwa kwa uzembe.
Dk
Kalemani amesema hayo leo Alhamisi Oktoba 26,2017 baada ya kukosekana
umeme nchi nzima jana Jumatano Oktoba 25,2017 kwa takriban saa 10, huku
kukiwa hakuna ufafanuzi wa kueleweka.
Waziri amemtaka meneja huyo kuandika barua ya kujieleza ndani ya saa tatu ni kwa nini asiondolewe katika nafasi hiyo.
Dk
Kalemani pia amempa siku tatu Meneja Udhibiti wa Mitambo, Mhandisi
Izihaki Mosha kujieleza ni kwa nini anastahili kubaki katika nafasi
hiyo.
Mbali
na maagizo hayo, waziri amemtaka Ikwasa; Naibu Mkurugenzi Usafirishaji,
Mhandisi Bishaija Kahitwa na Mosha kuandika barua za kuachia nafasi zao
iwapo umeme hautarudi siku nzima leo.
“Siwaondoi, bali nataka umeme usiporudi muondoke wenyewe katika nafsi zenu kwa sababu hii kazi itakuwa imewashinda,” amesema.
Dk
Kalemani amesema, “Haiwezekani umeme ukatike nchi nzima ndani ya saa 10
na bado hamjajua tatizo ni nini, wananchi wanatuma ujumbe mfupi kila
kona wameunguliwa vitu vyao, wameunguliwa mashine zao nani atalipa hizo
gharama.”
Waziri
aliyefanya ziara kwenye mitambo ya kuzalisha umeme Ubungo na Kinyerezi I
jijini Dar es Salaam kubaini chanzo cha kukatika kwa umeme nchi nzima,
amesema wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umekwisha.
Amesema haiwezekani kusiwe na spea za akiba za mitambo ambayo ni muhimu katika uzalishaji wa umeme.
Dk
Kalemani amehoji iwapo kulikuwa na hitilafu kwenye gridi ya Taifa ni
kwa nini mashine nyingine nazo zipoteze mwelekeo huku kukiwa na kitengo
cha mfumo wa uendeshaji.
“Hakuna
haja ya kuwa na mfumo ambao hautoi taarifa mapema kama kuna tukio
hatarishi linakuja, ninachotaka kusikia ni nini kifanyike ili tuwe na
taarifa mapema,” amesema.
Waziri
amesema, “Kila mnaloulizwa hamjui, mnasubiri hadi mitambo iharibike
ndipo mchukue hatua, nchi haiwezi kuendeshwa hivyo, kukosa umeme ndani
ya saa 10 ni hatari kwa mali za raia lakini kwa usalama pia. ”
“Sitaki kubishana hilo ndilo neno ninalowaacha nalo leo, nataka umeme urudi nchi nzima, hii haiwezekani,” amesema Dk Kalemani.
Pia, ameagiza mkandarasi anayeshughulikia mfumo wa utendaji wa umeme ambaye yupo nje ya nchi kurudi nchini.
“Nataka awepo kazini kesho na sitaondoka kuelekea Dodoma hadi nijue hatima ya mkandarasi, ” amesema.
Post a Comment
karibu kwa maoni