Anaandika Benny Mwaipaja, Dodoma
MAKAMU
wa Rais Mhe. SAMIA SULUHU HASSAN, amezinduzi Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo ya Fedha ya
mwaka 2017 na Mkakati wa Utekelezaji wake katika kipindi cha miaka 10 kuanzia
2017/2018 hadi mwaka 2027/2028, tukio litakalofanyika Makao Makuu ya Wizara ya
Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Makamu
wa Rais ametoa wito kwa watoa huduma ndogo
za fedha kupunguza riba za mikopo na tozo mbalimbali ili kufanikisha
lengo la Sera hiyo ambalo ni kuimarisha huduma jumuishi za fedha kwa
kujenga mazingira wezeshi yatakayoleta ufanisi wa utoaji wa huduma ndogo
za
fedha nchini kwa wananchi wenye kipato cha chini.
“Ninawaomba pia muongeze ubunifu katika kutoa
huduma zinazohitajika na wananchi wa kipato cha chini pamoja na kupeleka huduma
hizo katika maeneo yaliyo karibu na
makazi yao au biashara zao” aliongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan
Alizitaka taasisi za huduma za fedha kuwaelimisha
wananchi kabla ya kutoa huduma hizo ili kupunguza athari wanazozipata wananchi.
“Ni matarajio
yangu kuwa, Wizara ya Fedha na Mipango itashirikiana na wadau katika kutekeleza
Sera hii na kuhakikisha malengo ya Sera
ambayo ni kukuza uchumi na kupunguza umaskini
yanafikiwa” alisisitiza
Alisema Ripoti
ya Finscope ya mwaka 2017 ambayo iilionesha kuwa Tanzania imepiga hatua kwenye
suala zima la huduma jumuishi za fedha (financial inclusion) na kufikia
asilimia 72 kwa 2017, huku changamoto kuu iliyoainisha ni elimu/uelewa mdogo wa
huduma za fedha kwa wananchi.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango alisema kuwa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017
na Mkakati wa Utekelezaji wake itaweka
mazingira yatakayowezesha kuchochea maendeleo stahiki na ubunifu wa Huduma
Ndogo za Fedha ili kukidhi mahitaji halisi ya wananchi wa kipato cha chini na
hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Alisema kuwa Sera hiyo itaongeza
utoaji wa huduma bora na jumuishi ya Kifedha Vijijini na kutungwa kwa sheria ambazo
zitawalinda wananchi dhidi ya baadhi ya taasisi za kifedha zinazoibuka na kuwa
kero kwao kwa kuweka riba kubwa pamoja na kupatiwa huduma zisizoridhisha.
“Sera ya
Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 na Mkakati wa Utekelezaji wake vitaendelea
kutoa miongozo kwa wadau wote na kuchochea uanzishwaji wa washiriki wapya na
ukuaji wa waliopo ili kutoa ushindani zaidi ili kuleta matokeo yatakayoongeza
huduma rasmi, kukuza utamaduni wa kuweka akiba, kuimarisha sekta ndogo ya
fedha, ambayo yatachangia ukuaji wa uchumi, ajira na kupunguza umaskini”
Aliongeza Dkt. Mpango
Sekta ya huduma ndogo ya fedha nchini inajumuisha aina
ya watoa huduma za fedha wafuatao: benki na taasisi za fedha zinazotoa huduma
ndogo za fedha; vyama vya ushirika wa kuweka akiba na
kukopa; kampuni za huduma ndogo za fedha kama vile BRAC, Blue Finance,
Tujijenge, Platinum n.k,
Nyingine ni asasi za fedha zisizo za
Serikali, Mifuko na Programu za Serikali; na
Vikundi vya Kifedha vya Kijamii kama vile asasi za kijamii, benki za
kijamii za vijiji (VICOBA), Ushirik a wa akiba na mikopo vijijini (VSLAs),
Ushirika wa akiba na mikopo kwa zamu
(ROSCAs), wakopeshaji binafsi na wengine
wanaotoa huduma zinazohusiana na fedha.
Serikali
kwa kutambua umuhimu wa upatikanaji wa Huduma Ndogo za Fedha kwa wananchi wa
kipato cha chini iliamua kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za
Fedha ya Mwaka 2000 kwa kutunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka
2017 na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo kwa kipindi cha miaka kumi ili
kutatua changamoto zilizojitokeza katika sekta ndogo ya fedha
Changamoto hizo ni pamoja na ongezeko la idadi ya watoa Huduma
Ndogo za Fedha; Ukosefu wa mfumo wa Sheria na Kanuni za kusimamia Taasisi
Zisizochukua Amana na Vikundi vya Fedha vya Kijamii; Ukosefu wa mfumo wa
kumlinda Mtumiaji na mtoa Huduma Ndogo
za Fedha na uelewa mdogo wa masuala ya
fedha; Kutokuwepo na uwazi katika vigezo
na masharti ya utoaji mikopo; Viwango
vya juu vya riba; na Kuibuka kwa taasisi zisizo kuwa na uaminifu.
Post a Comment
karibu kwa maoni