0
Kamishna wa Madini nchini, Benjamin MchwampakaKAMPUNI ya TanzaniteOne na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) wamefanikiwa kuuza madini yenye thamani ya Sh bilioni 1.8 katika mnada uliofanyika kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Naisinyai kilichopo wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Kampuni ya TanzaniteOne na Stamico wameweza kuuza madini hayo kwenye mnada wa madini ulioshirikisha wanunuzi wa madini kutoka kampuni mbalimbali za madini hayo za ndani na nje ya nchi.
Awali kampuni mbili za wazawa ambazo ni Tanzanite Africa Ltd na ClassicGame Ltd walijitokeza kuuza madini hayo lakini waliyaondoa kutokana na kutoridhika na bei iliyokuwa sokoni na hatimaye Kampuni za TanzaniteOne na Stamico walifanikiwa kuuza madini hayo.
Akitangaza matokeo ya mnada huo, Kamishna wa Madini nchini, Benjamin Mchwampaka alisema kuwa jumla ya gramu 47,201. 00 za tanzanite ghafi ziliuzwa kwa dola za Marekani 820,744. 00.
Alisema kutokana na mauzo hayo serikali inatarajia kukusanya mrahaba na ada ya ukaguzi dola za Marekani 57,452.08 sawa na Sh milioni 128.8. Alisema pia Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro inatarajia kulipwa Sh milioni 5.5 kwa kodi na huduma.Image result for TANZANITE
Naye Naibu Waziri wa Madini, Stanislaus Nyongo alisema wanampongeza Rais John Magufuli kwa kutangaza mnada huo wa madini kufanyika mkoani Manyara ili kufungua fursa za biashara katika eneo hilo.
Pia alisisitiza kuwa suala la kudhibiti utoroshwaji wa madini hususani ya tanzanite ni mojawapo ya hatua zilizochukuliwa, ikiwemo kujengwa kwa ukuta kwa kuzunguka eneo la mgodi ya tanzanite wenye urefu wa kilomita 24.5.
Alitoa rai kwa wachimbaji wa madini kuhakikisha wanashiriki katika mnada huo mara kwa mara ili waweze kuuza madini yao ya tanzanite. Awali Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema kuwa kampuni 12 zinazochimba madini ya tanzanite eneo la Mirerani zinadaiwa kiasi cha Sh bilioni 3 baada ya kudiriki kukwepa kulipa kodi serikalini.
Alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukuliwa hatua za kisheria wachimbaji wengine wa madini hayo ya tanzanite kwani ni lazima walipe kodi ili waweze kufanya biashara zao. Naye mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya TanzaniteOne, Hussein Gonga aliipongeza serikali kwa kuwezesha mnada huo kufanyika kwa mara ya kwanza kwenye eneo hilo na kufungua fursa ya biashara kwa wakazi wa eneo hilo.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top