WANACHAMA
139 wa Chadema wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wamejiunga
na CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Manyara Mosses
Komba.
Akizungumza
wakati wa kuwapokea na kuwakabidhi kadi za CCM wanachama hao wapya,
Komba alisema wamefanya uamuzi sahihi kwa wakati sahihi. Komba
alisema hawatajuta kujiunga na CCM kwani hivi sasa chama hicho
kinachoongozwa na Mwenyekiti wake Rais John Magufuli kinawatumikia
wananchi kwa kutatua kero na kuufanikisha maendeleo.
Alisema
wanakaribishwa CCM kwa moyo mmoja hivyo washirikiane na wanachama
wengine ili kuhakikisha wanalirudisha jimbo hilo na kata sita
zinazotawaliwa na Chadema. "Kati
ya makosa tuliyofanya kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ni kuachia
jimbo la Simanjiro liende Chadema na kata za Mirerani, Naberera,
Loiborsiret, Ruvu Remit, Loiborsoit na Endiamtu zichukuliwe na
wapinzani," alisema Komba.
Alisema
ushabiki wa kufuata mkumbo ndiyo uliowagharimu wananchi wa wilaya hiyo
na kata hizo, hadi kusababisha wakapatikana madiwani na mbunge wa kutoka
upinzani badala ya CCM."Nakuagiza
Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya ya Simanjiro, Thomas Mollel na wenyeviti
UVCCM wa kata husika ambazo madiwani wao ni wapinzani, mkishindwa tena
2020 mjiuzulu," alisema Komba.
Mwenyekiti
wa UVCCM wa wilaya ya Simanjiro Thomas Mollel alisema kwa kushirikiana
na vijana wenzake wa Simanjiro, watahakikisha wanatekeleza agizo hilo la
kurejesha jimbo na kata sita zinazoshikiliwa na wapinzani. "Hata
hivyo, wananchi wengi wa Simanjiro wana imani kubwa na Rais John
Magufuli kupitia CCM mpya, tunatarajia uchaguzi ujao wa mwaka 2020
tutarudisha jimbo na kata hizo sita," alisema Mollel.
Alisema
vijana ndiyo nguzo kubwa ya ushindi kwenye chama hicho na wamepata
mwamko wa kushiriki kuwajulisha wananchi kuwa CCM ndiyo chama cha
kukimbilia. Mjumbe
wa baraza la utekelezaji UVCCM mkoa wa Manyara, Elizah Ladis alisema
tangu waanze ziara ya kutembelea wilaya za mkoa huo mwezi Desemba mwaka
jana, hiyo ndiyo idadi kubwa ya wapinzani 139 kujiunga na CCM.
"Simanjiro
wametupokea kwa wapinzani 139 kujiunga na CCM wilaya za Hanang na
Mbulu, wapo waliojiunga ila siyo wengi kama hawa, tunaelekea Kiteto na
Babati sasa tunatarajia kupata wapinzani wengine," alisema Ladis.
Post a Comment
karibu kwa maoni