Februari 28, 2018: Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania ruzuku ya Yen bilioni 3.78 sawa na Shilingi bilioni 77.3 kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo
yametiwa saini Februari 28, 2018, Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali, na Balozi wa Japan
nchini Tanzania Masaharu Yoshida na kushuhudiwa na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la
Maendeleo la Japani (JICA), Toshio Nagase na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini-Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale.
Mradi wa barabara hiyo yenye
urefu wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa
awamu ya nne ya ujenzi wa barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka
(BRT phase IV).
Akizungumza baada ya kutiwa saini
wa makubaliano hayo, Bw. Doto James amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika
itasaidia kutatua changamoto ya
msongamano wa magari yanayotoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
"Upanuzi wa Barabara ya New
Bagamoyo si tu kwamba utaondoa msongamano wa magari, bali pia ni kiungo muhimu
cha Bandari ya Bagamoyo ambayo itarahisisha usafirishaji wa abiria, mizigo na
huduma kutoka Jiji la Dar es Salaam, mkoa wa Pwani na mikoa mingine
nchini" Alisema Bw. Doto James.
Ameishukuru Japan kwa msaada
mwingine uliotolewa mwezi Septemba, 2017 wa kiasi cha fedha za Japan (Yen)
milioni 69 sawa na shilingi bilioni 1.4 ambazo zimetumika kwa ajili ya kufanya
upembuzi yakinifu wa barabara hiyo itakayoanza kujengwa
Bw. James ameeleza kuwa awamu ya kwanza, Japan ilitoa kiasi cha
shilingi bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne katika kipande cha kilometa
12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na makutano ya barabara ya Mwenge
pamoja na kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Mlalakuwa, Lugalo na Tegeta.
“Si mara ya kwanza kwa Japan
kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara, ujenzi
wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km
188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi
Dodoma (259.9)” alisisitiza Bw. Doto James.
Balozi wa Japan, Mhe. Masaharu
Yoshida ameeleza kuwa kutolewa kwa msada huo ili kuwezesha awamu ya pili ya
ujenzi wa barabara kuanza kutayafanya matokeo ya kujenga barabara hiyo kuanza kuonekana
dhahiri ikiwemo kupunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa ili kuokoa
fedha nyingi zinazotokana na changamoto za msongamano huo.
"Ili kukamilisha usanifu wa
kina wa mradi huu, nilisaini mkataba wa usanifu wa kina wa mradi wa upanuzi wa
barabara ya new Bagamoyo (Awamu ya Pili)
miezi mitano iliyopita, hatimaye sasa ninasaini mkataba wa sehemu kuu ambayo ni
ujenzi wenyewe" Alisema Balozi Yoshida.
Balozi huyo wa Japan hapa nchini,
amesema mradi huo utasaidia kuboresha ukuaji wa uchumi na kupunguza
umasikini nchini na kwamba msaada huo ni mwendelezo wa kudumisha uhusiano mzuri
uliopo kati ya Japan na Tanzania.
Utafiti uliofanyika hivi karibuni
unaonesha kuwa Barabara ya Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa magari yanayokadiriwa 52,000 yanayopita kila siku
katika barabara hiyo.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Post a Comment
karibu kwa maoni