Baraza
Kuu la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) jana
Jumamosi Aprili 7, 2018 limetoa tamko lenye mambo saba, likiwemo la
kupinga uamuzi wa Serikali kuwafuta kazi watumishi wake wenye elimu ya
darasa la saba.
Akisoma
tamko hilo mbele ya wajumbe wa baraza kuu la Tucta katika mkutano wa
baraza hilo uliofanyika mkoani Morogoro mwenyekiti wa Tucta, Tumaini
Nyamhokya alisema uamuzi huo wa Serikali si sahihi na hivyo wametaka
watumishi hao kurejeshwa kazini.
Alisema baraza limesikitishwa na uamuzi wa kuwaondoa kazini watumishi wa umma na taasisi zinazopokea ruzuku kutoka serikalini.
Nyamhokya alisema uamuzi huo si wa kisheria ikizingatiwa kuwa watumishi hao waliajiriwa kwa kufuata taratibu halali za ajira.
“Kwa
hiyo Tucta tunaitaka serikali kutengua uamuzi wake na kuwarudisha
watumishi hao kazini bila kupoteza haki zao za kiutumishi kwa kipindi
chote,” alisema.
Mambo
mengine sita yaliyopo katika tamko hilo wanayotaka yafanyiwe kazi ni;
ongezeko la mishahara, kodi ya mishahara (PAYE), kupandishwa madaraja na
vyeo kwa watumishi wa umma, malimbikizo ya mishahara kwa wafanyakazi na
watumishi kwa baadhi ya taasisi, ucheleweshwaji wa malipo ya wastaafu
kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii na uamuzi wa Serikali
kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii.
Post a Comment
karibu kwa maoni